Arusha. Baadhi ya mila na imani potofu, zimetajwa kuathiri huduma za matibabu ya saratani kwa jamii na kusababisha kuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la wagonjwa wa saratani kufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo, hali inayopunguza uwezekano wa kupona na kuongeza gharama za matibabu.
Aidha wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani,wanatarajia kuondokana na adha ya kufuata huduma za magonjwa ya saratani katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma au Hospitali ya Rufaa ya KCMC (Moshi) baada Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mt. Meru kuanza matibabu hayo.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Aprili 10, 2026 na Meneja wa Programu wa Mradi Mtambuka wa kupambana na Saratani kwa wanawake Jumuiya ya Afrika Mashariki (EA-CwCP), Dk Sarah Maongezi, wakati wa uzinduzi wa huduma za tiba ya kemikali katika Hospitali ya Mt. Meru.
Uzinduzi wa huduma hizo umekwenda sambamba na Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan (AKHS) chini ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), kukabidhi vifaa vya tiba kemikali vyenye thamani ya zaidi ya Sh58 milioni vitakavyotumika katika huduma hizo za tiba kemikali.
Amesema katika kutoa matibabu ya saratani miongoni mwa changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo ni mila pofotu ambapo mgonjwa anafika hospitali akiwa amechelewa na kuishia kwenda kutibiwa kw waganga wa jadi.
Amesema wagonjwa wengi huchelewa kufika hospitalini kutokana na kuamini tiba za jadi au ushauri usio sahihi kutoka kwa jamii, na hivyo kupoteza muda muhimu wa kuanza matibabu mapema.
“Mtu anakuja ameshachelewa na unamshauri kwenda hospitali lakini bado anakwenda kwa waganga wa kienyeji, wengi tumewaibua kutoka kwa waganga ila tunaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma ngazi za jamii ili wawasaidie wanaokutana nao na kuwapeleka hospitali,”
Ametaja changamoto nyingine ni uelewa wa jamii ambapo baadhi ya wanawake wanaokutwa na dalili za saratani hushindwa kuanza matibabu kwa madai kuwa wanaenda kuomba wenza wao ruhusa.
“Changamoto nyingine ni uelewa wa jamii,mtu unamwelewesha hii ni saratani lakini anakwambia anakwenda kuomba ruhusa kwa mwenza wake, hivyo anakosa maamuzi binafsi ya kutibiwa hadi akamuombe ruhusa mumewe.Ila saratani haisubiri, ukishagundulika inatakiwa kutibiwa ili isiendelee kwenye hatua nyingine,” amesema.
Dk Sarah amesema mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Taasisi ya Gates Foundation na AKDN na kutekelezwa kwa pamoja na Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Afrika Mashariki (Kenya na Tanzania) ambao kwa ujumla unagharimu Euro milioni 12.
Amesema mradi huo unalenga kuboresha huduma za saratani, kuongeza uelewa wa jamii na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa wakati,kuimarisha kinga,uchunguzi wa mapema na kuwa unatekelezwa katika mikoa sita nchini,Zanzibar, na Kaunti nne za nchini Kenya na kuwa Mt Meru ndiyo hospitali ya kwanza ya mkoa nchini kutoa matibabu hayo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mt Meru, Dk Alex Ernest, amesema jengo la huduma hiyo limejengwa na wadau binafsi kwa zaidi ya Sh 300milioni na litasaidia kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa saratani katika mkoa huo na maeneo jirani.
Amesema awali mkoa wa Arusha mgo njwa akitambulika kuwa na saratani alikuwa analazimika kwenda Hospitali jijini Dar Es Salaam au KCMC Moshi,na ambao hawakuwa na uwezo walijikuta wakiendelea kushambuliwa na ugonjwa huo na kufikia hatua ambayo hawezi kupona isipokuwa kupata matibabu saidizi.
“Tunashukuru wadau wetu Aga Khan kwa kutupatisa vifaa tiba ambavyo vimewezesha leo tumeanza kutoa matibabu hapa ambapo siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wengi kutokana na utambuzi wa wagonjwa,hivyo lazima matibabu yatolewe kwa haraka pia,”
“Kwa kutambua hilo mkoa uliweka juhudi za kupata mfadhili aliyetusaidia kujenga jengo hilo na kuanza kutolewa hduuma kutasaidia wananchi wa mikoa ya kaskazini kwani KCMC ilikuwa ikielemewa kwani ndiyo pekee ilikua inatoa huduma hii katika ukanda huu huku wengine wa mkoa wa Manyara waliokuwa wakienda Benjamin Mkapa (Dodoma).
Naye Mwakilishi wa Hospitali ya Aga Khan Tanzania, Murtazan Mukhtar,ametaja vifaa tiba hivyo ni pamoja na viti maalum vya wagonjwa (recliners), pampu za kudunga dawa (infusion pumps) na vifaa vya usalama wa kibaolojia, vyote vikilenga kuboresha huduma za tiba ya kemikali na usalama wa wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya.
Amesema lengo ni kushirikiana na serikali kuimarisha huduma za afya nchini na kupunguza adha ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Kwa upande wake daktari bingwa wa saratani kutoka Aga Khan Dar es Salaam, Dk Morris Chuwa, amesema wataalamu wa hospitali hiyo wamepatiwa mafunzo ya kutosha kuhakikisha huduma zinazotolewa zina ubora.
Amesema saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa wanawake nchini, huku saratani ya matiti ikiongezeka kwa kasi hasa kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 40.
“Tumetoa mafunzo kwa madaktari ili wahakikishe wanatoa hduuma salam ningependa kuwahakikishia wananchi kuwa kwa mafunzo ambayo tumewapa mafunzo yanayofuata miongozo,”amesema Dk Chuwa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Dk Jacob Rombo, alipongeza wadau kwa mchango wao na kueleza kuwa huduma hizo zimekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaongeza juhudi za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Alisema huduma hizo zitasaidia wagonjwa kupata matibabu kwa wakati, kurejea katika hali zao za kawaida na kuendelea kuchangia maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla ambapo aliwataka watoa huduma kutimiza wajibu wao kwa moyo.
