Mkurugenzi Olympafrica afichua mkakati wa kukuza vipaji Zanzibar

WAKATI Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiboresha miundombinu ya michezo kisiwani hapa, wadau wa michezo wameanza kuwajenga watoto kukuza vipaji vyao.

Katika kufanikisha hiyo, Kituo cha Olympafrica kilichopo Dole kimekuwa na utaratibu wa kuandaa mechi za kirafiki kwa watoto zenye lengo la kujenga uhusiano bora baina yao.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo iliyochezwa Aprili 8, 2026 kwenye uwanja wa kituo hicho, Mkurugenzi wa Olympafrica, Hussein Ahmada amesema wanaandaa mechi hizo kupata vijana wenye uwezo wa kujiunga kwenye vyuo vinavyokuza watoto ikiwemo hapo.

“Dhumuni la kuandaa mechi za aina hiyo ni kuwapa watoto uzoefu na kujenga uhusiano mzuri baina yao,” amesema.

Pia, Mkurugenzi huyo, alitoa wito kwa Taasisi mbalimbali kujitokeza kuwasaidia vijana wa aina hiyo ambao wanaonesha kuwa tayari kucheza mpira.

Amesema, taasisi zinapojitokeza zitakuwa na uwezo wa kuwasaidia vijana ikiwemo vifaa ili kuwakuza katika maadili mazuri na yenye mustakabali mwema kwa maisha yao.

Mechi hiyo imechezwa kati ya vijana kutoka Mtaa wa Beit-rasi na kituo cha Olympafrica Zanzibar ambapo, Beit-rasi imeibuka na ushindi wa bao 1-0.