KOCHA Mkuu wa Muembe Makumbi City, Sheha Khamis amesema amefurahishwa kuona kikosi chake kimeondoka ugenini kisiwani Pemba na alama nne katika mechi mbili za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Hatua hiyo imemfanya kocha huyo kuwapongeza vijana wake kwa kazi nzuri waliyoifanya kuipambania timu hiyo kutopoteza ugenini katika harakati za kufikia malengo yao msimu huu.
Ikiwa Pemba, Muembe Makumbi ambaye maskani yake yapo Unguja, ilicheza michezo miwili kwenye Uwanja wa Gombani ikizifunga Junguni mabao 6-1 na kuambulia matokeo ya 0-0 mbele ya Chipukizi.
“Siku zote mechi za kisiwani Pemba zinakuwa ngumu kupata matokeo mazuri, lakini wachezaji wangu walivyopambana na kucheza kwa kufuata maelekezo wanastaili pongezi,” amesema.
Amesema awali timu hiyo ilikuwa na mkakati ya kuondoka na alama sita, lakini sio mbaya kupata nne na kuacha mbili.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kupambana na kufakiwa kuvuna alama hizi, bila ya hivyo ingekuwa kinyume chake, naamini tutaendelea na kiwango hiki katika michezo nane iliyobaki ya ligi na michuano ya FA Cup inayotukabili,” amesema.
Kocha huyo amesema msimu huu malengo yao ni kumaliza ndani ya nne bora na kuchukua ubingwa wa FA Cup ili washiriki mashindano ya kimataifa.
Baada ya kuvuna alama hizo nne, Muembe Makumbi City imefikisha 33 ikishika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo unaoongozwa na Fufuni yenye alama 41.
Kocha Sheha amesema kwa sasa anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa FA Cup hatua ya 16 bora dhidi ya JKU utakaochezwa Aprili 15, 2026.
