Dar es Salaam. Mtandao wa kijamii wa Instagram umetangaza kuja na kipengele kipya ambacho kitawawezesha watumiaji wake kufanya marekebisho ya maoni wanayoyaandika kwenye machapisho mbalimbali.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni majibu ya hitaji la muda mrefu la watumiaji wa mtandao huo ambao awali walilazimika kufuta maoni yaliyokuwa na makosa na kuandika upya.
Hata hivyo, huduma hiyo imekuja na masharti kadhaa, ikiwemo ukomo wa muda ambapo mtumiaji atakuwa na dakika 15 pekee za kufanya marekebisho hayo tangu muda aliochapisha maoni yake.
Baada ya dakika hizo kupita, mtumiaji hatakuwa na uwezo wa kubadilisha chochote.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Instagram mtandao wenye watumiaji zaidi ya bilioni tatu, leo Aprili 10, 2026, marekebisho hayo yatahusisha maandishi pekee.
Hii ina maana kwamba ikiwa maoni yana picha na maandishi, mtumiaji ataweza tu kubadili maneno na si picha iliyoambatanishwa.
Licha ya ukomo wa dakika 15, mtumiaji anaruhusiwa kufanya marekebisho mara nyingi kadiri awezavyo ndani ya muda huo.
Ili kuleta uwazi, Instagram imebainisha kuwa maoni yoyote yatakayofanyiwa marekebisho yataonyesha alama ya “Edited” (imefanyiwa marekebisho) ili watumiaji wengine wafahamu kuwa kilichoandikwa awali kimebadilishwa.
Hata hivyo, tofauti na baadhi ya mitandao mingine, Instagram haitaonyesha kumbukumbu ya kile kilichoandikwa awali (version history), hivyo kulinda faragha ya mhusika kuhusu makosa aliyoyafanya kabla ya kurekebisha.
Mabadiliko haya ni mwendelezo wa maboresho ambayo Instagram imekuwa ikifanya katika ushindani wa soko la mitandao ya kijamii, ikichuana na majukwaa kama X (zamani Twitter) na Facebook ambayo tayari yana huduma kama hizo.
Hatua hii imekuja ikiwa ni miaka mingi tangu Instagram ilipoanza kuruhusu uhariri wa maelezo ya picha (captions) mwaka 2014. Wadau wa masuala ya teknolojia wanaona hatua hii kama namna ya Instagram kwenda sambamba na washindani wake kama mtandao wa X (zamani Twitter) na ule wa Threads ambao tayari una huduma hiyo.
Kwa sasa, huduma hii inaanza kusambazwa kwa watumiaji kote duniani na inatarajiwa kuwafikia watu wote kwenye mifumo ya Android na iOS ndani ya muda mfupi.
