Global Publishers
April 10, 2026
0 Comments
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa onyo kali kwa uongozi wa Iran kufuatia taarifa kuwa nchi hiyo inaendelea kutoza ada kwa meli za mafuta zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Akizungumza, Trump amesema kuwa vitendo hivyo vinapaswa kusitishwa mara moja, akisisitiza kuwa vinaweza kuathiri usafirishaji wa mafuta duniani na kuongeza mvutano wa kimataifa.
“ Kuna ripoti kwamba Iran inatoza ada kwa meli za mafuta zinazopita Hormuz waache mara moja,” alisisitiza.
Ripoti zinaeleza kuwa meli nyingi za mafuta zimeanza kuchelewa au kusita kupita katika eneo hilo muhimu la kimkakati kutokana na gharama hizo pamoja na ukosefu wa mwongozo wa wazi kutoka mamlaka za Iran kuhusu utekelezaji wa utaratibu huo.
Hatua hiyo inakuja baada ya Bunge la Iran kupitia Tume yake ya Usalama kuidhinisha mpango wa kutoza ushuru kwa meli zinazopita katika mlango huo wa bahari, jambo ambalo limezua wasiwasi mkubwa katika sekta ya nishati duniani.
Wachambuzi wanasema kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, hivyo hatua yoyote ya kuongeza vikwazo inaweza kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta na kuathiri uchumi wa kimataifa.
Hadi sasa, haijabainika wazi ni lini au kwa kiwango gani Iran itaanza rasmi kutoza ada hizo, huku wadau wa usafirishaji wakisubiri maelekezo rasmi kutoka serikalini.