Umuhimu wa ujenzi wa imani katika jamii ya Kiislamu

Tatizo la jamii ya Kiislamu leo hii, si ukosefu wa mwonekano wa kidini au ukosefu wa misikiti, au udhaifu wa mawaidha.

Minara ya misikiti na majukwaa ya kuhubiri yamekuwa mengi, tatizo lipo katika mwonekano wa nje wa Waislamu na kukosekana utekelezaji wa imani ya kweli.

Watu wengi utawakuta wanatimiza ibada vizuri, lakini wanakosea katika utekelezaji wa upande wa muamala, na utakuta wengine wanajitahidi katika upande wa utekelezaji wa Sunna lakini wanasahau upande wa haki na maadili. Hivyo tunahitaji kujipamba na imani ya kweli itakayohuisha njia ya wema waliotangulia katika ujenzi wa utu wa muumini.

Uislamu unaiweka dini katika mchanganyiko wa kulazimiana na mambo ya dhahiri na siri.

Ibada lazima izalishe tabia njema; tabia isiyozalishwa na imani sahihi haina faida katika Uislamu Allah Mtukufu amesema: “Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa aya zake huwazidisha imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. (Quran 8: 2).

 Hivyo aya imeitaja imani ni hali ya moyo inayotafsiriwa kwa matendo. Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake) amesema: “Hakika ndani ya mwili kuna kipande cha nyama, kikitengamaa kipande hicho, basi mwili wote hutengemaa, na kikiharibika kipande hicho basi mwili wote huharibika, kipande cha nyama hicho ni moyo”

Moyo uliosafi huzalisha matendo yote safi, na kinyume chake moyo uliopotea unasababisha uharibifu wa matendo yote..

Tatizo linakuja pale mtu katika hali ya dhahiri anayeonekana kwa macho anatimiza ibada za swala, swaumu n.k, lakini anakuwa na tabia ngumu pindi anapochangamana na wenzake, au katika utekelezaji wa haki za watu, anakuwa si mwaminifu licha ya kuwa anaswali na kufunga sana.

Mtume wa Allah amesema: “Huenda mfungaji Swaumu hana anachopata katika swamu yake isipokuwa kushinda na njaa.Na huenda anayesimama usiku kuswali hana anachopata isipokuwa kukesha tu”

Hadithi hii inasisitiza kuwa na nia safi kwa Allah katika kila ibada, na kuepukana ibada isiyo na matokeo mazuri katika maisha ya Muislamu ya kila siku.

Kuna sababu nyingi zinazochangia dini iwe katika mwonekano wa nje tu, bila ya ya kuleta matokeo ya imani ya kweli: Mosi, udhaifu katika kujifunza elimu ya sharia, kusoma elimu ya dini ni lazima (faradhi) na ibada kubwa.

Anayeipuuza na kutoijali elimu ya dini anajikosesha nafasi ya heshima. Allah Mtukufu amesema: “Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni mwenu, na waliopewa ilimu daraja za juu… ” (Quran 58: 11).

Pili, udhaifu katika utakaso wa nafsi Allah amesema: “Hakika amefaulu yule aliyetakasa nafsi yake” (Quran 91: 9). Kwa bahati mbaya, utakaso wa nafsi haujazingatiwa katika hutoba nyingi, au haukupewa umuhimu mkubwa unaolingana na maana ya wema waliotangulia (salaf swalih).

Utakaso wa nafsi unafanywa kwa mujibu wa muongozo wa Mtume wa Allah, Ibn al-Qayyim amesema: “Utakaso wa nafsi ni mgumu zaidi kuliko kutibu mwili; kama mtu anataka kujitibu kwa mbinu zake, anaweza kushindwa…”

Tatu, kuzingatia dhahiri ya nje kuliko malengo husika. Watu wengine wamejikita tu kwenye taswira ya nje ya ibada, wamesahau malengo yake ya asili, ikiwemo ikhlas, ukweli, na huruma. Mtume wa Allah alisema: “Hakika matendo yote huzingatiwa kwa nia, na kila mtu atapata kulingana na alivyokusudia” (Bukhari na Muslim). Ibada bila nia ya kweli haiwezi kustawi. Nne, upungufu katika mihadhara ya ulinganiaji. Baadhi ya mihadhara inapitiliiza mipaka katika ukali unaosabaibisha ushadadiaji (ghuluw) na kuogopesha watu, au urahisishaji uliokithiri unaosababisha udhaifu katika kufuata amri ya dini. Allah amesema: “Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli….”   (Quran 4: 171)).

Mfumo wa wema waliotangulia (salaf Swalih) katika ujenzi wa imani, unajenga utu wa muumini kwa msingi thabiti wa mchanganyiko wa imani na tabia, elimu na matendo, Ibada na maadili .

Hii si imani ya maneno tu, wala si elimu iliyohifadhiwa bila tija; imani lazima itafsiriwe katika maneno, moyo, na vitendo.

Tauhidi (kumpwekeksha Allah) ndio asili ya dini na wajibu wa kwanza ni kumwabudu Allah peke yake. Hii ndiyo njia ya manabii wote: “Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu. (Quran 21: 25).

Kufuata Mtume: Bila kufuata Mtume (Rehema na amani ziwe juu yake), dini haiwezi kustawi; kumtii Mtume ni sehemu ya kumtii Allah. Kutii mwenendo wake ni njia ya kuokoka, na kupuuza kwake ni mlango wa kufuata bid‘a (uzushi).

Mtume wa Allah amesema: “Shikamaneni na mwenendo wangu na mwenendo wa Makhalifa waongofu.” Mfumo huu unatoa mfano wa imani iliyo sawa, inayofanya mtu kuwa bora, na jamii iwe na maadili mema.

Sheikh Seif Ruga: 0712 690811