…….
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataarifu wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuwa, Aprili 12, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chamwino, Jimbo la Mvumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 10, 2026 jijini Dodoma, Senyamule amesema kuwa ziara hiyo inalenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi, kusikiliza changamoto zao, pamoja na kutoa maelekezo ya Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii na maendeleo katika maeneo husika.
Ameeleza kuwa ziara hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi wa Wilaya za Bahi na Chamwino kuwasilisha kero zao moja kwa moja kwa Waziri Mkuu, huku akisisitiza umuhimu wa ushiriki mpana wa wananchi katika mikutano itakayofanyika.
“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili wapate nafasi ya kuwasilisha maoni na changamoto zao, jambo litakalosaidia Serikali kuchukua hatua stahiki kwa maendeleo yao,” amesema Senyamule.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, utulivu na ushirikiano katika kipindi chote cha ziara hiyo, akibainisha kuwa hali hiyo itachangia kuimarisha taswira ya Mkoa wa Dodoma kama kitovu cha shughuli za kitaifa na fahari ya Watanzania.