Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere imebaini asilimia 99.92 ya wazee wasiojiweza nchini hawapati huduma za malezi ya kijamii ikiwemo afya, makazi, lishe, ushauri nasaha na huduma nyinginezo muhimu k.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya ukaguzi kuhusu utoaji wa huduma za ustawi wa jamii kwa wazee kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyowasilishwa bungeni Aprili 10, 2026.
Ripoti hiyo inaonyesha kati ya wazee 633,758 wanaohitaji huduma za kijamii kutokana na hali zao duni za maisha, ni 488 pekee wanaofikiwa na huduma hizo, huku wazee 633,270 wakibaki bila msaada wowote.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, changamoto zaidi ipo katika maeneo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambako asilimia 99.99 ya wazee wasiojiweza hawapati huduma hizo kabisa.
Kwa upande wa Kanda ya Mashariki, ambayo imeonekana kuwa na nafuu kidogo, ni asilimia 4.38 tu ya wazee wanapata huduma za kijamii.
Katika ripoti hiyo, CAG Kichere anasema alibaini nyumba zote 13 za makazi ya wazee hazikidhi viwango vilivyopendekezwa ikiwemo miundombinu rafiki kwa wazee kama vyoo maalumu, sakafu zisizoteleza na mifumo ya huduma za dharura.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali hiyo imesababishwa na udhaifu katika mipango, upangaji bajeti na utekelezaji wa mipango ya ukarabati au matengenezo ya nyumba hizo.
“Aidha, ukaguzi umebaini kati ya Sh820 milioni zilizopangwa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba tano za wazee katika kipindi cha miaka mitatu, ni nyumba moja tu ya Ipuli iliyofanyiwa ukarabati kutokana na kuchelewa au kutotolewa kwa fedha za bajeti,” imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inaeleza hali hiyo imesababisha baadhi ya nyumba kubaki na miundombinu chakavu.
Katika upande wa rasilimali watu, ripoti imeonyesha upungufu wa wataalamu muhimu ikiwemo wataalamu wa lishe, mazoezi ya viungo, ofisa ugavi, dereva katika nyumba zote 13 za wazee, jambo linaloathiri utoaji wa huduma muhimu kwa kundi hilo.
Pia, ripoti hiyo imebainisha wafanyakazi wa nyumba za wazee hawajapata mafunzo ya mara kwa mara kwa kipindi cha miaka mitano, hali inayowafanya kukosa ujuzi wa kisasa wa kuwahudumia wazee hasa katika afya ya akili, lishe na msaada wa kisaikolojia.
Ripoti hiyo ya CAG imebaini kuwepo kwa uzingativu mdogo wa ubora na virutubishi katika chakula kinachotolewa kwa wazee katika makazi yao.
Aidha, hakukuwa na programu maalumu za mlo kwa wazee wenye changamoto maalumu za kiafya kama vidonda vya tumbo, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kisukari.
“Hali hii ilichangiwa na mgao mdogo wa bajeti ya chakula pamoja na tofauti za aina ya vyakula vinavyotolewa katika makazi ya wazee.
Hali hiyo imetajwa kuwaweka wazee katika hatari ya kupata utapiamlo, kupungua uzito, kudhoofika kwa kinga ya mwili na ongezeko la uwezekano wa kupata magonjwa.
Ripoti hiyo pia imebaini upungufu mkubwa wa vifaa saidizi katika makazi ya wazee. Uhaba ulibainika katika vifaa vya mwendo na visaidizi vya kusikia ikiwemo fimbo 38 za kutembelea, mikongojo 15 na vifaa vya kusikia 10.
Upungufu huo ulisababishwa na kutofanyika kwa tathmini ya mahitaji halisi ya vifaa saidizi katika kila makazi ya wazee pamoja na kukosekana kwa mikakati na bajeti maalumu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
CAG amesema kwa mujibu wa matokeo ya ukaguzi, mfumo wa utoaji huduma za malezi kwa wazee nchini bado hauna ufanisi wa kutosha, hali inayowafanya wazee wengi kukosa huduma muhimu za kijamii na kiafya.
Ripoti hiyo imeeleza hali hiyo inahitaji hatua za haraka za kisera na kiutendaji ili kuhakikisha wazee wanapata huduma bora, zenye kuzingatia mahitaji yao halisi.
Katika mapendekezo yake, CAG ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kuandaa miundombinu bora ya makazi ya wazee pamoja na kusimamia ukarabati wa mara kwa mara wa nyumba hizo ili ziendane na mahitaji ya wazee.
Pia, CAG amependekeza kuwepo kwa mipango ya lishe yenye virutubisho vya kutosha kwa wazee wanaoishi katika makazi hayo ili kuboresha afya zao.
Aidha, ripoti hiyo imeitaka wizara hiyo kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na usimamizi wa huduma ili kuhakikisha ubora wa huduma unazingatiwa kwa karibu.
