CAG afichua mambo mawili kirusi kwa mashirika ya umma

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema mashirika 22 kati ya 54, sawa na asilimia 41, yanaendelea kujiendesha kwa hasara kutokana na uwekezaji usio na tija, gharama kubwa za uendeshaji na udhaifu wa mifumo ya udhibiti wa ndani.

Akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni Aprili 10, 2026, CAG amesema hali hiyo pia inachangiwa na uwezo mdogo wa taasisi hizo kuzalisha mapato ya ndani na utegemezi mkubwa wa ruzuku za Serikali, jambo linalotishia uimara wa kifedha wa muda mrefu.

Takwimu zinaonesha ongezeko la mashirika yanayopata hasara kutoka asilimia 37 (taasisi 19 kati ya 52) mwaka 2023/24 hadi asilimia 41 (taasisi 22 kati ya 54) mwaka 2024/25, huku hasara ya jumla ikifikia Sh307.1 bilioni.

“Sababu kuu za kuongezeka kwa hasara hizi zinaendelea kuwa ni utendaji duni, mapato hafifu ya uwekezaji na udhaifu katika udhibiti wa matumizi,” amesema.

Mashirika yanayoongoza kwa hasara

Ripoti hiyo imetaja taasisi kadhaa, zikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kampuni ya Ndege Tanzania, UDART, Mkulazi, Ranchi za Taifa, Kiwanda cha Biolojia Tanzania, Kampuni ya Jotoardhi Tanzania, TTCL Pesa, Kiwanda cha Dawa Keko, Tanapa Investment, STAMIGOLD na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC).

Kampuni ya Ndege Tanzania imeongoza kwa hasara ya Sh191.19 bilioni, kutoka Sh91.79 bilioni mwaka uliopita, licha ya kupokea ruzuku ya Sh114 bilioni. Shirika la Reli Tanzania nalo limeendelea kukabiliwa na changamoto za ufanisi, huku UDART likirekodi hasara ya Sh15.78 bilioni.

Kwa upande wa Reli ya Kati, shehena ya mizigo imeshuka kutoka tani 302,714 hadi 246,824, hali iliyopunguza mapato ya shirika hilo.

Ruzuku za Serikali na utegemezi

Ripoti inaeleza kuwa ruzuku za Serikali zimeongezeka kutoka Sh29.08 bilioni hadi Sh137 bilioni, lakini bila kuleta ufanisi wa moja kwa moja. CAG amesema kupungua kwa jumla ya hasara kutoka Sh412.31 bilioni hadi Sh307.10 bilioni kumetokana zaidi na ruzuku za uendeshaji badala ya maboresho ya kiutendaji.

Aidha, Serikali imewekeza Sh159.60 bilioni kupitia ruzuku za maendeleo, lakini CAG ameonya kuwa utegemezi huo umegeuka kuwa mzigo wa kudumu badala ya suluhisho la matatizo ya ufanisi.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa mashirika 49 yana uwiano wa ukwasi kati ya 0.00 hadi 0.98, ishara ya kushindwa kulipa madeni ya muda mfupi.

Pia, mashirika 16 yasiyo ya kibiashara yanaendelea kujiendesha kwa upungufu wa kifedha kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku matumizi yasiyo na tija yamefikia Sh117.62 bilioni katika taasisi 16, ingawa yamepungua kwa asilimia 68 ukilinganisha na mwaka uliopita.

Hata hivyo, matumizi yasiyostahili yameongezeka hadi Sh8.56 bilioni, yakihusisha malipo yasiyoendana na sheria, mikataba na viwango vya uhasibu.

Kwa Kampuni ya Ndege Tanzania, changamoto zimehusishwa na gharama kubwa za matengenezo ya ndege, mishahara, ukodishaji, safari zenye abiria wachache na ushindani wa soko la kimataifa.

CAG ameonya kuwa bila mageuzi ya ufanisi, mashirika ya umma yataendelea kuwa mzigo kwa Serikali na kuongeza hatari ya kuyumba kwa uchumi wa nchi.

Ili kuondokana na hali hiyo, CAG amependekeza kuharakishwa kwa uandaaji na utekelezaji wa mifumo ya usimamizi wa vihatarishi pamoja na sera za kuzuia udanganyifu.

Aidha, ameshauri kuanzishwa kwa rejesta za vihatarishi zinazorekodi na kufuatilia hatari zote pamoja na hatua za kuzidhibiti, sambamba na kufanya tathmini za mara kwa mara na kuwasilisha taarifa kwa bodi za wakurugenzi wa ndani ili kuhakikisha uwajibikaji na uimara wa taasisi za umma.