Dodoma. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi ametaja kuwa kinachowaumiza waliowachagua viongozi ni matumizi mabaya ya imani waliyopewa na wananchi.
Dk Nchimbi amesema viongozi wengi wamekuwa wakitumia madaraka yao kwa kujinufaisha wenyewe badala ya kuyatumia kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Aprili 11, 2026, wakati akizungumza kwenye kongamano la vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuadhimisha miaka 104 ya kuzaliwa kwake.
Amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa dhamana wanayopewa ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si kwa manufaa yao binafsi, kwani wananchi wanatarajia aliyepewa dhamana atumie madaraka kwa maslahi yao, lakini katika maeneo mengi imekuwa kinyume.
Dk Nchimbi amewataka viongozi kuiga mfano wa Hayati Mwalimu Nyerere ambaye anatajwa kuwa alikuwa kiongozi wa mfano mwenye uadilifu na uzalendo, aliyechukia rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa vitendo, na alihakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na kubaki kwa manufaa ya Watanzania wote.
Amesema licha ya Nyerere kushika nafasi ya urais, aliishi maisha ya kawaida yasiyo na ubadhirifu, jambo lililojenga heshima kwake ndani na nje ya nchi, hadi akawa kiongozi wa mfano kwa Afrika na dunia.
“Misingi ya umoja, mshikamano na amani iliyoasisiwa na Baba wa Taifa ndiyo nguzo muhimu ya taifa, lakini vitendo vya ubaguzi wa kidini, kikabila na kupuuza usawa katika jamii, pamoja na kuruhusu baadhi ya watu kuwanyima wengine haki, vinaweza kusababisha mpasuko katika jamii, na jambo hilo Mwalimu hakulipenda,” amesema Dk Nchimbi.
Kiongozi huyo amewahimiza vijana kujihoji kama wako tayari kulinda amani ya nchi, kupinga rushwa na kutumia elimu waliyoipata kwa maendeleo ya taifa badala ya maslahi binafsi.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo, ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amewataka vijana kutokata tamaa na kujifunza kwa viongozi waliotangulia, akisisitiza umuhimu wa kujenga taifa lenye viongozi waadilifu watakaotumikia wananchi kwa haki.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel, amewataka vijana kubadilika kifikra na kuwa na uthubutu, lakini watumie changamoto kama fursa, akionya kuwa maamuzi mabaya ya sasa yanaweza kuwaathiri baadaye.
