Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi amewataka viongozi wa dini kushirikiana kwa karibu katika juhudi za kupambana na mmomonyoko wa maadili, akisisitiza endapo hautadhibitiwa, unaweza kuwa tishio kubwa kwa jamii.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo leo Jumamosi Aprili 11, 2026 imeeleza kuwa Katambi ametoa wito katika kikao kazi na viongozi wa dini chenye ajenda ‘mmomonyoko wa maadili, amani na utulivu, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
“Hakuna bomu baya kuliko silaha za kivita kama mmomonyoko wa maadili, jambo hili linaathiri kila kukicha, nawaomba viongozi wa dini mtusaidie sana kulipiga vita,” amesema.
Waziri Katambi amesema hivi sasa familia hazitekelezi wajibu wake kwa kiwango kikubwa, hasa vijana huku akifurahia kuona wazee wakihakikisha Taifa linakuwa na amani na usalama kutokana na kulelewa katika maadili mema.
“Vijana wenye maadili mazuri wapo, sio tatizo kwa sababu wanabeba ile hofu ya Mungu. Lakini tukiacha mmomonyoko wa maadili uendelee kushamiri katika jamii tafsiri yake hatutokuwa salama,” amesema Katambi.
Katika hatua nyingine, Katambi amesema milango ipo kwa viongozi wa dini kwa lengo la kushauriana na kupokea maoni yanayolenga kudumisha tunu ya amani itakayohakikisha utulivu wa nchi.
Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Ally Ngeruko amemshukuru Katambi kwa kuuandaa kikao hicho chenye lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na mmomonyoko wa maadili.
