KUNA viungo wawili wamewaka pale Yanga wakipiga mabao na asisti lakini kocha mmoja aliyewahi kufundisha Simba amemtaja mmoja akisema huyo Allan Okello kama ameshaanza balaa hilo, timu pinzani zijiandae kwani atafanya makubwa.
Iko hivi; kwenye mabao saba ambayo Yanga imeyafunga katika mechi zake tatu zilizopita, Okello amehusika kwenye mabao matano kwa kufunga na kupiga asisti kwa wafungaji wengine.
Kama haitoshi kwenye mabao hayo ametengeneza kombinesheni moja ya moto kati yake na kinara wa ufungaji kwenye timu hiyo Mudathir Yahya na wameshirikiana kwenye mabao manne.
Mabadiliko hayo ya Okello yanakuja wakati ambao kocha wa timu yake, Pedro Goncalves akimbadilishia matumizi akimrudisha kucheza kama namba 10 badala ya kushambulia akitokea pembeni alikokuwa anacheza kabla kisha kuonekana hana madhara.
Lakini, Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira akaona makali ya Okello kwenye mechi ya juzi dhidi ya Pamba alipopiga hat trick ya asisti, Yanga ikishinda 3-0 ugenini akisema sasa ndiyo balaa la kiungo huyo linaanza.
Robertinho ambaye aliwahi kufanya kazi Uganda wakati Okello akiwa anacheza ligi ya kwao, amesema alikuwa anajua kiungo huyo mara atakapoanza kutumika kama namba 10 basi atafanya makubwa kutokana na ubora wake wa kujua kutengeneza nafasi.
“Nilikwambia kabla Yanga wanavyomtumia Okello pembeni hawataona faida yake, nimeona hizi mechi mbili wamempanga anapotakiwa kucheza, nadhani unaona sasa faida ya Okello kucheza hapo, anapika mabao na kufunga,” amesema Robertinho.
“Nilikuwa namwona Okello Uganda, ilikuwa ni ngumu kukabiliana na timu yake akicheza eneo hilo, ana akili kubwa sana ya kutengeneza nafasi na mkimsahau anawafunga, hapa sasa Yanga watafurahia usajili wake lakini huu sio uamuzi mzuri kwa wapinzani watakutana na wakati mgumu sana kuizuia Yanga.
Kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, Okello ameshaifungia Yanga mabao mawili lakini akitengeneza jumla ya asisti nne akiongoza kwenye timu hiyo, akihusika kwenye jumla ya mabao sita kwenye timu yake akiwa ameingia usajili wa dirisha la Januari 2026.
Aidha Robertinho alifichua wakati akiwa Simba aliwahi kumtaja kiungo huyo asajiliwe kwa wekundu hao bahati mbaya klabu yake iligoma kumuachia.
“Nikiwa Simba kuna wakati tulikuwa tunatafuta nani anaweza kuja kuziba nafasi ya Chama (Clatous), tuliona kama Chama anahitaji kutafutiwa mtu mwingine endapo tutamkosa, nikawaambia viongozi wamsajili Okello, viongozi walinisikia lakini klabu yake ikagoma kumuachia,” amesema.
Wakati Robertinho akiyasema hayo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amechekelea kiwango cha Okello akisema amekuwa akionyesha kushirikiana vizuri na Mudathir Yahya kwenye eneo la mwisho na kuzalisha madhara kubwa kwa wapinzani.
“Tunafurahia kiwango cha Okello, unaona namna wanavyoshiriana na Mudathir (Yahya) ,wote wako kwenye kiwango kizuri, wanabadiliushina na kutengeneza ubunifu mzuri wa nafasi ambazo tunatengeneza,” amesema Pedro.
Mudathir ndiye kinara wa ufungaji Yanga akiwa na mabao saba na asisti moja, akiwashusha washambuliaji Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambao wamefunga mabao sita kila mmoja.
