Kombe la FA: Yanga kuivaa TMA Stars, Coastal Union uso kwa uso na Pamba Jiji

LIGI Kuu Bara imesimama kidogo na utamu unahamia Kombe la Shirikisho la CRDB na bingwa mtetezi Yanga inarudi uwanjani kutafuta hesabu za kulinda taji lake itakapokuwa mwenyeji wa wabishi wa Arusha, TMA Stars.

Yanga imeonyesha haitaki masihara kwenye kutetea taji hilo ikitoka kuiangamiza Polisi Tanzania mabao 7-1 hatua ya 32, Machi 8, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex ambao ndio utatumika tena dhidi ya TMA.

Yanga kwenye ushindi wa mabao 7-1 ulizalisha hat trick yake ya kwanza msimu huu ikiwekwa na mshambuliaji wake Laurindo Aurelio ‘Depu’ lakini kocha wa timu hiyo Pedro Goncalves ameonyesha hana jambo dogo akimwaga mastaa wake wakubwa kwenye mechi hizi.

Mchezo huo wa hatua ya 16 Yanga hata hivyo italazimika kuwa makini na TMA inayofundishwa na staa wa zamani wa Azam FC, Haji Nusu, ikitoka kuishtua Prisons kwao kwa kuichapa kwa bao 1-0 lililowapeleka hatua inayofuata.

Ukuta wa Yanga ambao umeruhusu bao moja unatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Ernest Baltazari ambaye ndiye aliyezamisha jahazi la Prisons kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Halmashauri ya Chunya, jijini Mbeya.

Yanga inaweza kuwa na mabadiliko machache kwenye kikosi chao ikitaka kulinda afya za wachezaji wake kutokana na kukabiliwa na wimbi la majeruhi wengi wakati ikiwa kwenye hesabu ngumu kwenye ligi.

Akizungumzia mechi huo, Pedro amesema timu yake inakwenda kucheza tofauti, ikipitia njia ngumu ya kuwakosa wachezaji wake muhimu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi ili kujiweka salama kwenda kutetea taji lao.

“Kesho (leo) tunakwenda kukutana na TMA timu inayotoka ligi ya daraja la kwanza, tunafahamu inapitia pia wakati mgumu kwenye ligi yao itahitaji kutafuta unafuu kwenye mashindano haya, tunapitia pia wakati mgumu kutokana na kuwakosa wachezaji wetu lakini bado tunatakiwa kufanya vizuri, nimewaambia wachezaji tunatakiwa kujituma na kuwajibika sawasawa kwenye mchezo huu,” amesema Pedro.

Kocha wa TMA, Omary Matiko amesema timu yake imejiandaa vizuri, ikitambua ukubwa wa Yanga na itatumia mpango kazi wao kutafuta ushindi kwenye mchezo huo wa hatua ya mtoano.

“Kimsingi tumejindaa vizuri huku tukijua ukubwa wa Yanga, aina ya ligi wanayocheza kulinganisha na yetu ni vitu viwili tofauti, tumejiandaa kwa mpango kazi wa mchezo huu tukijua kwamba ni mchezo wa mtoano, tunatakiwa kuwa makini,” amesema Matiko.

Mbali na mchezo huo pale Tanga wenyeji Coastal Union ikiwa bila kocha mkuu Mohammed Muya aliyeachana na klabu hiyo, itakuwa mwenyeji wa Pamba Jiji kila timu ikitafuta nafasi ya kusonga mbele.

Coastal Union itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kuichapa Stand United kwa mabao 4-1 yakifungwa na kiungo Cleofas Mkandala aliyepiga mabao mawili huku mengine yakifungwa na winga Shiza Kichuya na mshambuliaji Abdulkarim Segeja.

Pamba ikitoka kupoteza nyumbani kwenye ligi itataka kuwafuta machozi mashabiki wake baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani msimu huu mbele ya Coastal Union, ikitoka kuing’oa Transit Camp kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na mshambuliaji Henry Lutonja na winga John Nakibinge.