Miloud Hamdi arejea kazini Misri, akabidhiwa Al Ittihad

KLABU ya Al Ittihad ya Misri imefikia makubaliano ya kumwajiri kocha wa zamani wa Yanga, Miloud Hamdi, mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, ikiwa ni miezi miwili tangu alipojiuzulu kuifundisha Ismaily SC, Januari 26, 2026.

Miloud aliyeipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la CRDB msimu wa 2024-2025, alijiuzulu Januari 26, 2026, baada ya mwenendo mbaya wa kikosi hicho cha Ismaily SC kutoka Misri, tangu alipojiunga nacho Julai 3, 2025.

Taarifa kutoka Misri, zinaeleza Miloud atawasili muda wowote kuanzia sasa katika Jiji la Alexandria, kwa lengo la kukamilisha makubaliano hayo, huku ikielezwa atawasili na kocha msaidizi mmoja.

Mbali na kupewa ruhusa ya kuja na msaidizi wake, Miloud amewekewa mkataba wa kukiongoza kikosi hicho hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026, huku kukiwa na kipengele kitakachomruhusu kuongeza kandarasi ya mwaka mmoja.

Katika kipindi cha miezi sita cha Miloud akiwa na Ismaily SC, aliiongoza timu hiyo kucheza mechi 19 za mashindano tofauti, ambapo alishinda nne, sare mbili na kupoteza 13, huku kikosi hicho kikifunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26.

Kwa msimu huu wa 2025-2026, katika Ligi ya Misri, Al Ittihad imecheza mechi 20, imeshinda sita, ikitoka sare mbili na kupoteza 12, huku ikiwa imefunga mabao 15 na kuruhusu 24, ikishika nafasi ya 15 kwenye msimamo, kati ya timu 21, ikikusanya pointi 20.

Februari 4, 2025, Miloud alitua Yanga akitokea Singida Black Stars iliyomtambulisha Desemba 30, 2024.

Hamdi aliyezaliwa Juni 1, 1971, ana leseni ya Ukocha ya UEFA Pro, akizifundisha Al-Khaldiya SC ya Bahrain, JS Kabylie, CS Constantine na USM Alger za (Algeria), Al-Salmiya SC (Kuwait), RS Berkane (Morocco) na Al Ittifaq ya Saudi Arabia.