BAADA ya kushuka daraja msimu wa 2024-2025, Mwenge SC ya kisiwani Pemba sasa mipango ni kuvunja ukuta ili kurejea Ligi Kuu Zanzibar.
Katika mipango hiyo, inahitaji pointi 13 pekee katika mechi saba zilizobaki za Ligi Daraja la Kwanza, Kanda ya Pemba zitakazoifanya kurejea kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Pemba imebakiwa na raundi saba, hivyo timu hiyo inatakiwa kushinda mechi nne na sare moja kati ya hizo ziliizobaki.
Kwa sasa timu hiyo imekusanya pointi 52 baada ya michezo 23, huku matumaini ya kurejea Ligi Kuu yakiimarika.
Kinara wa ligi hiyo, Wembe tayari imekusanya pointi 61, ikibakiwa na nne tu kuweka hesabu sawa ya kupanda daraja.
Hesabu hizo zinakuja baada ya kanuni za ligi hiyo kutoa nafasi ya timu mbili za juu kupanda daraja na sasa Wembe na Mwenge ndizo zipo hapo.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Wawi Stars yenye pointi 44, hivyo ina kibarua kizito cha kuhakikisha inashinda mechi zote saba, kisha kuziombea mabaya hizo mbili za juu ili yenyewe ipande na mmoja kati yao.
Hesabu za mechi hizo saba na Wawi anapaswa kushinda zote, zitamfanya kumaliza msimu na pointi 65 ambazo kwa sasa Wembe ikishinda mechi moja na sare moja, inazifikia, huku ikiwa na mwanya mkubwa wa kuzipita kufuatia idadi ya michezo iliyobaki.
Mwenge yenyewe ikishinda mechi nne na sare moja itafikisha pointi 65, hivyo pia ina wigo mpana wa kuzivuka kwani ina michezo saba ya kumaliza msimu huku ikiwa na wastani mzuri wa kushinda unaombeba.
