Global Publishers
April 11, 2026
0 Comments
Baada ya kufanikiwa kwa misheni ya Artemis II na kurejea salama kwa wanaanga wake, Shirika la anga la Marekani (NASA) sasa linaelekeza nguvu zake kwenye hatua inayofuata misheni ya Artemis III inayotarajiwa kuzinduliwa mwaka 2027.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa safari hiyo, Rick Henfling, alisema NASA tayari imeanza maandalizi ya safari hiyo mpya kwa kutumia uzoefu walioupata kutoka Artemis II.
“Tutachukua mafunzo yote tuliyojifunza kutoka Artemis II. Tumejifunza mambo mengi kuhusu kusafirisha binadamu angani, kuendesha mifumo ya chombo cha anga, na hata namna ya kusimamia kituo cha udhibiti wa safari za anga za mbali,” alisema Henfling.

Katika misheni ya Artemis III, NASA inapanga kufanya majaribio ya chombo cha kutua Mwezini (lunar lander) kitakachotengenezwa na kampuni za SpaceX au Blue Origin, au zote mbili, wakati kikiwa katika obiti ya Dunia.
Hatua hii inalenga kuhakikisha teknolojia hiyo inafanya kazi ipasavyo kabla ya kutumika katika safari za kutua Mwezini.
Misheni ya Artemis II iliweka historia kwa kuwa safari ya kwanza yenye binadamu kuvuka obiti ya chini ya Dunia tangu mwaka 1972, kipindi cha mwisho cha safari za Apollo program.
NASA inalenga kurejesha binadamu kwenye uso wa Mwezi kupitia misheni ya Artemis IV mapema mwaka 2028, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa uchunguzi wa anga, unaojumuisha pia maandalizi ya safari za kuelekea sayari ya Mars.