RPC Mutafungwa atangaza vita kwa watumia mihadarati Ukerewe

Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa ametangaza operesheni maalumu na isiyo na ukomo dhidi ya wahalifu wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na matukio ya uvunjifu wa amani katika Wilaya ya Ukerewe.

Mutafungwa ametoa kauli hiyo Aprili 10, 2026 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kagunguli, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, uliowahusisha wananchi, viongozi wa dini na watumishi wa Serikali, baada ya kubainika kuwepo kwa changamoto ya vijana kujiingiza kwenye dawa za kulevya na uhalifu.

Katika kutatua kero hizo, Kamanda Mutafungwa amemwagiza Mkuu Polisi Wilaya ya Ukerewe, Elija Matiko kwa kushirikiana na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Wilaya, kuimarisha misako na doria katika maeneo yote ili kusambaratisha magenge ya wahalifu.

“Tunataka maeneo yote wavuta bangi waanze kukamatwa; ninyi ndiyo mliotuambia kuwa bangi imezidi hapa, sasa nami nataka kazi ianze kufanyika mara moja,” amesema Mutafungwa.

Aidha, ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza hususani wa Wilaya ya Ukerewe, kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa za siri kuhusu wahalifu.

Amebainisha kuwa jukumu la ulinzi na usalama ni la pamoja kati ya vyombo vya usalama na wananchi na kwamba ushirikiano huo ndio nguzo kuu ya kutokomeza uhalifu kuanzia ngazi ya vitongoji na kata.

Mkazi wa Kagunguli, Fedelia James amepongeza maamuzi hayo akisema yameleta matumaini ya kurejea kwa amani ya kudumu.

“Wananchi wanapokuwa na matatizo wawe wanatoa taarifa kwa vyombo husika hususani serikali za vijiji, mitaa na hata polisi kwa utatuzi wa matatizo kwa uharaka ili kuepusha matatizo makubwa hapo baadaye,” amesema Anthony Bili, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.

Amewahimiza wananchi kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa, badala yake wawasilishe taarifa za watu hao kwenye mamlaka husika ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.