SERIKALI YATAKA MAGEUZI YA HARAKA KUBORESHA HUDUMA ZA MAHUJAJI WANAOKWENDA HIJJA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Alhaj Hemed Suleiman Abdulla ametoa maelekezo kwa Taasisi zinazohusika na uratibu wa Ibada ya Hijja kwa mwaka 2026, kufanya mageuzi ya kimfumo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa Mahujaji 4,029 kutoka Tanzania. 

Mhe. Abdullah amesema hayo katika Kikao kilichofanyika Visiwani Zanzibar leo ambapo amesisitiza umuhimu wa kuachana na mifumo ya kizamani na badala yake kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Aidha, ameelekeza kuanzishwa kwa mfumo wa Kanzidata (database) utakaokuwa na taarifa sahihi za Mahujaji hao ili kurahisisha mipango na utoaji wa huduma.

Pia, amesisitiza umuhimu wa Taasisi hizo kuzingatia maslahi ya taifa kwa kuepuka migongano ya kimaslahi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa usawa. Ameeleza kuwa maelekezo hayo yanapaswa kuanza kutekelezwa mara moja ili kuhakikisha maandalizi ya msimu wa Hijja 2026 yanafanyika kwa ufanisi ili kuimarisha taswira ya nchi kimataifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema kuwa Wizara imeendelea kusaidia uratibu wa Hijja kupitia kitengo chake cha Usajili wa Jumuiya na imefanikisha upatikanaji wa hati za kusafiria kwa Mahujaji hao, kwa ufanisi mkubwa ili kuhakikisha zoezi hilo la Maandalizi ya Ibada linafanyika kwa ukamilifu

Naye, Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amesema Idadi ya Mahujaji imeendelea kuongezeka, kutokana na ongezeko hilo kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maandalizi na uratibu wa safari hizo. Hivyo, Serikali imeanza kufuatilia maandalizi hayo kwa lengo la kuweka miongozo bora itakayosaidia kuhakikisha wanapata huduma na maelekezo sahihi wanapoelekea kutekeleza Ibada hiyo.