…………
Na Carlos Claudio, Dodoma
MCHUNGAJI wa Ushirika wa Mkonze, Emmanuel Jonathan Mwakabalila, amesema kuwa vijana ndio nguvu ya kanisa na taifa, akisisitiza kuwa vita ya kiroho inalenga zaidi kundi hilo kutokana na nafasi yao katika kuijenga kesho ya jamii.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kutangaza ibada maalum ya kusifu na kuabudu, Mchungaji Mwakabalila alisema kuwa mara nyingi changamoto za kiroho huwakumba vijana kwa sababu wao ndio wenye nguvu na mchango mkubwa katika maendeleo ya kanisa na jamii kwa ujumla.
“Vijana ndio wenye nguvu, na hata maandiko yanatambua hilo. Hakuna anayependa kitu dhaifu, hata ufalme wa Mungu unahitaji vijana imara ili kazi ya Mungu isonge mbele,” alisema.
Aliongeza kuwa ibada hiyo maalum itafanyika Jumapili, Aprili 12, 2026 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni katika viunga vya Kanisa la Moravian Ushirika wa Mkonze, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Pasaka.
Kwa mujibu wa Mwakabalila, tamasha hilo litahusisha kwaya mbalimbali na vikundi vya kusifu na kuabudu kutoka makanisa tofauti, likiwa na lengo la kuwafikia vijana na kuwavuta karibu na Mungu.
Alieleza kuwa katika ulimwengu wa sasa unaotawaliwa na teknolojia, vijana wengi wamejikuta wakivutwa na mitandao ya kijamii, kamari na shughuli nyingine zisizo na tija, hali inayohitaji juhudi za makusudi kuwarudisha kwenye misingi ya kiroho.
“Tunawaalika vijana waje madhabahuni wapokee uponyaji wa kiroho na kusikia neno la Mungu ili waweze kufunguliwa na kubadilika,” alisisitiza.
Kwa upande wake, muimbaji wa nyimbo za Injili na muinjilisti wa ushirika huo, Adam Kisimile, alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha ibada hiyo inakuwa na mguso wa kipekee kwa washiriki wote.
“Tunaamini madhabahu hii ina nguvu na watu wengi wamekuwa wakishuhudia matendo ya Mungu. Tunakaribisha kila mmoja aje apokee kile alichokikusudia moyoni,” alisema Kisimile.
Naye mzee wa kanisa hilo, Japhet Halinga, aliwahimiza wakazi wa Mkonze na Dodoma kwa ujumla kujitokeza kwa wingi, akibainisha kuwa sifa na kuabudu huvuta uwepo wa Mungu na kuleta uponyaji wa kiroho.
“Sifa zinafungua, zinaponya na zinamleta mtu karibu na Mungu. Hii ni fursa ya kipekee kwa kila mwenye uhitaji wa kiroho,” alisema.
Katibu wa Idara ya Vijana wa ushirika huo, Simon Mbaga, alisema kuwa maandalizi yamekamilika na vikundi mbalimbali vya kusifu na kuabudu vitashiriki kikamilifu katika ibada hiyo.
Alisisitiza kuwa lengo kuu la tamasha hilo ni kukuza imani, kuhamasisha ibada na kuwajenga vijana kiroho ili waweze kusimama imara katika maisha yao ya kila siku.
Aidha, muimbaji wa Injili Grace Kamendu aliwataka watu wa rika zote kushiriki, akisema kuwa ibada hiyo itakuwa ya kipekee na yenye baraka nyingi.
Alinukuu andiko kutoka Yoshua 1:9 linalohimiza ujasiri na kutokata tamaa, akisema kuwa Mungu yupo pamoja na kila mtu katika kila hali ya maisha.
Kwa pamoja, vijana wa timu za kusifu na kuabudu wa ushirika huo, akiwemo Mariam na Gloria Charles, waliwataka vijana kujitokeza kwa wingi, wakieleza kuwa kupitia sifa na kuabudu watu wengi wamekuwa wakiponywa na kufunguliwa.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Dodoma na maeneo ya jirani, huku waandaaji wakiahidi uwepo wa nguvu ya Mungu na mazingira rafiki ya ibada yatakayogusa maisha ya wengi.




