Visumbufu mimea, ndege kwereakwerea kudhibitiwa

Mbeya. Wakati msimu wa mavuno ya mpunga ukianza mkoani Mbeya, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini, (TPHPA) Nyanda za Juu Kusini imesema imejipanga kukabiliana na wadudu wasumbufu ambao hutokea kipindi cha msimu.

Pia, mamlaka hiyo imeeleza namna hatua inazochukua kukabiliana na wadudu wasumbufu katika mazao mbalimbali, ambao wamekuwa changamoto kwa wakulima na mimea kwa ujumla katika ukanda huo.

Kwa nyakati tofauti wakulima mkoani Mbeya na Songwe wamekuwa wakilia na wadudu aina ya funza weupe na konokono kushambulia mazao na kuharibu mashamba, hali inayoathiri uzalishaji na uchumi.

Ndege aina ya kwereakwerea wamekuwa wakidaiwa kutoka mataifa mbalimbali wakisafiri kwa makundi hadi wilayani Mbarali haswa kipindi cha msimu wa mavuno na kuharibu zao la mpunga na kuaingiza hasara wakulima.

Ndege aina ya kwereakwerea ambao hushambulia zao la mpunga inapofika wakati wa msimu wa mavuno

Mwaka 2025, TPHPA kwa kushirikiana na baadhi ya wadau wakiwamo shirika la kudhibiti ndege wa jangwani Afrika Mashariki (DLCO EA) waliweka kambi wilyani humo kwa ajili ya kukabiliana na ndege hao wasumbufu.

Akizungumza leo Jumamosi, Aprili 11, 2026 Meneja wa Mamlaka hiyo Nyanda za Juu Kusini, Pius Kawala amesema wakati msimu ukianza, Serikali imejipanga kuanzia vitendea kazi vya kisasa kuhakikisha wanawafikia wakulima.

Amesema Serikali tayari imenunua ndege na baadhi ya viuatlifu ambavyo vipo kila Mkoa, ambapo wanachosubiri ni kuona ndege hao wakifika na kuchukuliwa hatua akifafanua kuwa timu maalumu ya matukio ipo tayari.

“Sisi tumejipanga na kalenda ya matukio ikiwamo hao ndege kwereakwerea ipo, tumenunua tayari ndege, tunachofanya ni zile taarifa tunazopata tunaziripoti kitengo cha mlipuko kwa ajili ya kufanyia kazi,” amesema.

Wadudu aina ya konokono ambao hushambulia mazao ikiwamo kahawa ambao wamekuwa kero kwa wakulima haswa wilayani Mbozi mkoani Songwe.

“Tuna vikundi maalumu vyenye wakulima wazoefu kwa kushirikiana wataalamu wa TPHPA wanao jua malalo ya hao ndege tunapita nao maeneo yenye kwereakwerea hao kisha kitengo husika cha mlipuko kinakuja kudhibiti,” amesema Kawala.

Amewaomba halmashauri, wakulima na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano na haswa taarifa inapotokea majanga ya ndege hao na wadudu kuhakikisha mamlaka inachukua hatua za haraka ili kusaidia mkulima kuvuna kwa tija.

Kuhusu changamoto ya wadudu ambao wamekuwa kero wilayani Mbozi mkoani Songwe, Meneja huyo amesema wameendelea kuchukua hatua ikiwamo elimu na matumizi sahihi ya viuatilifu.

“Ipo mipango ya muda mfupi na muda mrefu, TPHPA inatarajia kuanza kutoa elimu kwa maafisa ugani wapya na wakulima japo zaidi ni kuzingatia ushauri wa kitaalamu juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu,” amesema Kawala.

Mmoja wa wakulima wa mpunga wilayani Mbarali, Shukuru Chaina amesema tayari wameanza mavuno ya mpunga tangu jana, ambapo ndege aina ya kwerea kwerea si wengi sana japokuwa huwa wanahama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.

“Tumeanza kuvuna jana ndege hawajawa wengi hali ya kutuathiri, japokuwa huwa wanahamahama, wanaweza kuwa wamekusanyika sehemu moja ghafla wakatuvamia muda wowote,” amesema.

“Kuhusu hali ya mpunga inashawishi tunaamini tunaweza kuvuna vizuri ila tatizo bei tuliyoanza nayo inatukata sana, gunia inauzwa kuanzia Sh 80,000 hadi Sh 90,000 tofauti na mwaka jana ilipoanzia Sh 120,000 hadi 165,000,” amesema Chaina.

Mkulima huyo ameongeza kuwa bei hiyo si rafiki sana kwa wakulima ikilinganishwa na gharama zinazotumika kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, palizi, mbolea hadi kuvuna.

Naye mkulima wa kahawa wilayani Mbozi, Isack Mwashivinga amesema wadudu aina ya konokono na funza weupe wamekuwa si rafiki katika ustawi wa mazao na kuathiri uchumi wa wakulima wanaotegemea kilimo.

“Tunaishukuru serikali kupitia TPHPA wamekuwa karibu na sisi na mara nyingi wametuletea sana watalaamu kufanya tafiti zao kujua changamoto, tunaomba watutafutie dawa za kumaliza wadudu hawa moja kwa moja,” amesema Mwashivinga.