Shirika la anga la Marekani, NASA, limethibitisha kuwa wanaanga wanne wa misheni ya Artemis II wako katika hali nzuri kiafya na wenye furaha baada ya kurejea salama Duniani kufuatia safari yao ya kihistoria angani.
Wanaanga hao walitua katika Bahari ya Pasifiki karibu na pwani ya California, tukio linalojulikana kama “splashdown,” kabla ya kuokolewa na kikosi maalum cha wanamaji kwa kutumia meli ya USS John P. Murtha.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika kituo cha Johnson Space Center, Mkurugenzi wa safari hiyo, Rick Henfling, alisema taarifa kutoka kwa madaktari zinaonesha kuwa wanaanga wote wako salama, wenye afya njema na katika hali nzuri ya kisaikolojia.

“Kwa mujibu wa taarifa tunazopokea kutoka kwa madaktari, wafanyakazi wa misheni wako na afya njema, wana furaha na wako tayari kurejea nyumbani Houston,” alisema Henfling.
Aidha, alibainisha kuwa rubani wa misheni hiyo, Victor Glover, alionekana akiwa katika hali nzuri na mwenye ari kubwa mara baada ya kuwasili kwenye meli ya uokoaji.

Baada ya kurejea Duniani, kipaumbele kikubwa kwa sasa ni kuhakikisha wanaanga wanarejeshwa haraka Houston ili kuungana na familia zao. NASA imeeleza kuwa wanatarajiwa kuwasili ndani ya siku hiyo, kati ya asubuhi na jioni, kulingana na ratiba ya safari.
Misheni ya Artemis II ni sehemu ya mpango mpana wa NASA wa kurejesha binadamu Mwezini kwa mara ya kwanza tangu enzi za safari za Apollo, pamoja na kuweka msingi wa safari za baadaye kuelekea sayari ya Mars.
Mafanikio ya kurejea salama kwa wanaanga hawa yanaongeza matumaini na kuimarisha hatua ya binadamu kuelekea uchunguzi wa anga za mbali zaidi.
