Chombo cha anga za juu cha Artemis II pamoja na wanaanga wake wanne kimepenya kwa kasi katika anga la dunia na kutua salama katika Bahari ya Pasifiki jana Ijumaa, baada ya kutumia takribani siku 10 angani kimehitimisha safari ya kwanza ya binadamu kuuzunguka mwezi katika kipindi cha zaidi ya nusu karne.
Chombo hicho cha Shirika la Anga la Marekani (Nasa), chenye umbo la duara kama pipi na kilichopewa jina la Integrity, kilishuka taratibu kwa kutumia miamvuli maalumu na kutua katika maji tulivu karibu na pwani ya Kusini mwa California saa 11:07 jioni kwa saa za Pasifiki.
Hatua hiyo ilihitimisha mpango ambao siku nne kabla uliwafikisha wanaanga umbali wa maili 252,756 kutoka duniani mbali zaidi kuwahi kufikiwa na binadamu angani.
Artemis II iliyosafiri jumla ya maili 694,392 (kilomita 1,117,515) ikijumuisha mizunguko miwili ya dunia na kupita karibu na mwezi umbali wa takribani maili 4,000 kutoka uso wake, ilikuwa jaribio la kwanza la safari ya kibinadamu katika mfululizo wa misheni za Artemis zinazolenga kuwapeleka wanaanga kwenye uso wa mwezi kuanzia mwaka 2028.
Tukio la kutua baharini lililofanyika chini ya anga lenye mawingu kiasi, lilirushwa mubashara kupitia matangazo ya Nasa. “Kutua sahihi kabisa kama kulenga shabaha na wanaanga wake wanne,” alisema mtangazaji wa Nasa, Rob Navias, alipozungumza na Reuters muda mfupi baada ya chombo hicho kugusa maji.
Dakika chache baadaye, kamanda wa misheni hiyo, Reid Wiseman, alitangaza kupitia redio: “Tuko imara wanaanga wote wanne wako salama,” akimaanisha kuwa chombo kilikuwa kimesimama vizuri na kila mwanaanga walikuwa katika hali nzuri.
Ilichukua chini ya saa mbili kwa timu za uokoaji za Nasa na Jeshi la Wanamaji la Marekani kukifikia chombo hicho, kukidhibiti na kuwaokoa wanaanga wote wanne wa Wamarekani Reid Wiseman (50), Victor Glover (49), Christina Koch (47), pamoja na Mkanada Jeremy Hansen (50).
Kurejea kwao ndiko kulikuwa kipimo kufanikiwa misheni hiyo na chombo cha Orion kilichotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin, kikithibitisha uwezo wa kinga yake ya joto kuhimili msuguano mkali wakati wa kurejea kutoka safari ya mwezini.
Chombo hicho kiliingia katika anga la dunia kwa kasi mara 32 ya sauti huku msuguano ukipandisha joto hadi nyuzi 5,000 za Fahrenheit (sawa na nyuzi 2,760 za Selsiasi). Wingu la gesi iliyochajiwa lilizingira chombo hicho na kusababisha kukatika mawasiliano kwa zaidi ya dakika sita jambo lililozua hofu kwa wafuatiliaji.
Hofu ilitulia baada ya mawasiliano kurejea, japo kwa kuchelewa kwa takribani sekunde 40 kuliko ilivyotarajiwa. Miamvuli miwili mikubwa ilifunguka kutoka mbele ya chombo hicho na kupunguza kasi yake hadi maili 15 kwa saa (takribani kilomita 25 kwa saa) kabla ya kugusa maji kwa utulivu.
Baada ya wazamiaji wa Jeshi la Wanamaji kufunga kifaa cha kukifanya chombo hicho kitulie juu ya maji, wanaanga hao, wakiwa bado wamevalia mavazi yao ya rangi ya machungwa, walisaidiwa kupanda kwenye mtumbwi wa mpira.
Kutoka hapo walichukuliwa mmoja baada ya mwingine kisha kuingia kwenye helikopta zilizokuwa jirani yao na kupelekwa kwenye meli ya kijeshi ya USS John P. Murtha (LPD-26) kwa uchunguzi wa afya.
Victor Glover na Christina Koch walionekana wakitabasamu na kupunga mikono. Wanaanga hao walitarajiwa kulala ndani ya meli hiyo usiku huo kabla ya kusafirishwa hadi Houston siku iliyofuata kukutana na familia zao.
Wanaanga hao wanne walirushwa angani kutoka Cape Canaveral, Florida, Aprili Mosi, wakitumia roketi kubwa ya Space Launch System ya Nasa, wakizunguka dunia mara mbili kabla ya kuelekea upande wa mbali wa mwezi ambayo ni safari ya nadra kufanywa na binadamu.
Kwa kufanya hivyo, walikuwa wanaanga wa kwanza kuuzunguka mwezi tangu enzi za mpango wa Apollo wa miaka ya 1960 na 1970.
Aidha, Victor Glover ameandika historia kwa kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza, Christina Koch mwanamke wa kwanza na Jeremy Hansen raia wa kwanza asiye Mmarekani kushiriki katika misheni ya mwezi.
Umbali wa juu walioufikia wa maili 252,756 ulivunja rekodi ya awali ya takribani maili 248,000 iliyowekwa mwaka 1970 na wanaanga wa Apollo 13.
