Wapinzani Zimbabwe wajawa hofu mabadiliko ya katiba yakishika kasi

Harare. Hofu imeongezeka miongoni mwa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe kwamba chama tawala cha Zanu-PF kinafanya jaribio jipya la kujiongezea madaraka huku kikisukuma mbele marekebisho ya Katiba yanayolenga kuipa Bunge badala ya wapigakura mamlaka ya kumchagua rais, pamoja na kuongeza muda wa uongozi kutoka miaka mitano hadi saba.

Mabadiliko hayo yanatazamwa kama mapinduzi dhidi ya nguvu ya umma huku wanasiasa wakieleza kuwa ni njama za chama tawala kuendelea kung’ang’ania madarakani bila ridhaa ya wananchi.

“Haya ni mapinduzi, mapinduzi ya polepole yanayoendelea nchini Zimbabwe,” amesema mwanasiasa mkongwe wa upinzani na aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Tendai Biti, akizungumza na BBC.

Hata hivyo, Zanu-PF ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru mwaka 1980, kimejitokeza kwa nguvu kutetea mabadiliko hayo.

“Hakuna kinachotuzuia kubadili mfumo na kwenda kwenye mfumo mwingine wenye gharama nafuu na usio na migogoro mikubwa,” amesema kiongozi wa chama hicho, Patrick Chinamasa.

Mitazamo hiyo kinzani inaonyesha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa uliosababishwa na muswada huo wa marekebisho ya Katiba, ukiwakutanisha uso kwa uso wafuasi wa Zanu-PF na wale wa upinzani.

Hali hiyo ilijitokeza wazi wakati wa vikao vya hadhara vilivyoandaliwa na Bunge hivi karibuni ili kuwapa wananchi nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo makubwa ya kikatiba.

Mabadiliko hayo yatakayojumuisha: kufutwa kwa uchaguzi wa rais ambao umefanyika tangu mwaka 1990, kuongeza muda wa wabunge na rais kutoka miaka mitano hadi saba na kuahirishwa kwa uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika 2028 hadi 2030.

Kwa maana hiyo, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, ambaye muhula wake wa pili na wa mwisho unatarajiwa kumalizika 2028, ataendelea kuwa madarakani hadi 2030. Vilevile, Bunge jipya kumchagua rais ajaye.

“Ninaunga mkono muswada huu kwa asilimia mia moja,” alisema mwanamke mmoja katika kikao cha hadhara kilichofanyika katika uwanja wa michezo jijini Harare wiki iliyopita.

Rais Mnangagwa aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya kumwondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu, Robert Mugabe kwa msaada wa jeshi, kabla ya kushinda uchaguzi uliopingwa mwaka 2018 na 2023.

“Muda wa uongozi uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba, na wabunge tunaowachagua wapewe mamlaka ya kumchagua rais,” alisema mwanaume mmoja katika kikao hicho kilichowakutanisha watu wenye maoni kinzani.

Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla pale kipaza sauti kilipoelekezwa kwa upande waliokaa wakosoaji wakuu wa muswada huo.

Kulizuka vurugu zilizofanana na zile ambazo mara nyingi zimekuwa zikichafua siasa za Zimbabwe—kusukumana, kupigana, pamoja na kunyang’anyana simu za mkononi na baadhi ya wanahabari kuamriwa kufuta video za tukio hilo.

Mwanasheria na mwanachama wa upinzani, Fadzayi Mahere aliiambia BBC kuwa wafuasi wa Zanu-PF walihusika na “vurugu” hizo ili kuwazuia wakosoaji kutoa maoni yao ya kupinga muswada huo.

Kwa upande wake, Patrick Chinamasa alikanusha madai hayo. “Tuna sababu gani sisi kama Zanu-PF kutumia vurugu wakati wananchi wako upande wetu? Upinzani haukubali kwamba hoja zao hazishindi,” alisema.

Hata hivyo, upinzani unasema kuwa Zimbabwe inashuhudia wimbi jipya la ukandamizaji. Kabla ya vikao hivyo, wanadai polisi walipiga marufuku zaidi ya mikutano 10 ya vyama vyao.

Kiongozi wa National Constitutional Assembly, Lovemore Madhuku alisema alipigwa na watu waliovaa barakoa mwezi uliopita huku polisi wakitazama.

Naye, Tendai Biti, ambaye anaongoza Jukwaa la Watetezi wa Katiba (Constitution Defenders Forum), yuko nje kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa kufanya mkutano wa hadhara bila kibali.

“Tuna historia ya ukandamizaji nchini Zimbabwe,” alisema.

Bunge linatarajiwa kupitisha muswada huo katika wiki zijazo, ikiwa ni kilele cha kampeni iliyoanza mwaka 2024, iliyoambatana na kaulimbiu ya “2030—bado atakuwa kiongozi”.

Kampeni hiyo ilikumbana na upinzani mkali hata ndani ya Zanu-PF, ingawa mkosoaji wake mkuu, Blessed Geza maarufu kama “Bombshell”, alifariki mapema mwaka huu.

Kwa wafuasi wa rais huyo mwenye umri wa miaka 83, mageuzi hayo ya kisiasa yataimarisha demokrasia kwa kumaliza kampeni za uchaguzi wa rais wanazodai mara nyingi husababisha vurugu na migogoro ya matokeo.