Arusha. Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa ya kupinga hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa fundi seremala, Alex Julius baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mpenzi wake, Kudura Hamis baada ya kujiridhisha ushahidi wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo.
Mwili wa Kudura ulikutwa chumbani ukiwa mtupu, umeanza kuoza Septemba 18, 2020 baada ya majirani kuanza kusikia harufu katika eneo la NHC Magadini, wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.
Uamuzi uliotupilia mbali rufaa hiyo ya Alex ulitolewa Aprili 10, 2026 na jopo la majaji watatu ambao ni Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 91, 2024.
Jaji Mwampashi amesema baada ya kupitia kwa kina hoja zote za rufaa pamoja na ushahidi uliowasilishwa katika Mahakama Kuu, wamejiridhisha kuwa hapakuwa na dosari yoyote ya kisheria iliyoweza kuathiri uhalali wa hukumu.
Amesema walibaini kuwa kifo cha marehemu kilithibitishwa kuwa si cha kawaida, bali kilisababishwa na kunyongwa, kwa kuzingatia ushahidi wa kitabibu uliotolewa bila kupingwa ipasavyo.
Aidha, walikubaliana na Mahakama Kuu kuhusu matumizi sahihi ya kanuni ya “mtu wa mwisho kuonekana na marehemu,” wakieleza kuwa mrufani alishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu tukio la mwisho kabla ya kifo hicho.
Majaji hao walisisitiza kuwa ushahidi wa kimazingira uliwasilishwa kwa uthabiti na uliunda mnyororo kamili unaoelekeza kwa mrufani pekee bila kuacha nafasi ya maelezo mbadala.
Awali mrufani alishtakiwa na kupatikana na hatia kwa kumuua Kudura kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu na baada ya kupatikana na hatia, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanane na vielelezo viwili ambapo ilidaiwa katika tarehe isiyojulikana, Alex alimuua mpenzi wake.
Shahidi wa pili na tatu ambao walikuwa majirani wa wapenzi hao, walidai walikuwa wakitembeleana katika makazi yao (mrufani na marehemu).
Kudura aliyekuwa akifanya kazi kama muhudumu wa baa, shahidi wa pili alidai Septemba 18, 2020 alisikia harufu mbaya kutoka kwenye chumba chake (Kudura) na kuwa mara ya mwisho alimuona Septemba 15, 2020.
Alidai akiwa ameambatana na wenzake, alifungua mlango wa nyumba hiyo ambao ulikuwa umefungwa kwa nje na waya na kuingia chumbani kwa Kudura ambapo walikuta mwili wake ukiwa umelala sakafuni.
Alidai mwili wa marehemu ambao ulikuwa mtupu na umeshaoza na kulikuwa na madoa makavu ya damu kwenye sehemu zake za siri, ambapo waliripoti kwa mwenye nyumba na kituo cha Polisi.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Kituo cha Afya cha Mto wa Mbu ambapo uchunguzi ulifanywa na Ofisa msaidizi wa matibabu, Verian Hosea aliyekuwa shahidi wa saba.
Shahidi huyo alieleza mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeanza kuoza ulikuwa na alama nyeusi usoni, majeraha kwenye mkono wa kulia karibu na kwapa, sehemu za siri zilizovimba na ulimi ukitoka kinywani mwake na kuhitimisha chanzo cha kifo ni kunyongwa.
Shahidi wa nne, aliiambia Mahakama kuwa Septemba 15, 2020 alikuwa kazini na marehemu na kuwa alimuona akiondoka na Alex ambaye ni mpenzi wake na alikuwa akimfuata hapo baa na kumsubiri baa ifungwe na kuondoka naye mara kwa mara.
Alidai siku hiyo saa nne ilikuwa mara ya mwisho kumuona Kudura, ambaye hakuwahi kuonekana kazini tena hadi Septemba 17, 2020 walipopata wasiwasi kuhusu alipo ambapo walikusanyika na shahidi wa nne na tano kupanga kumtafuta.
Alidai wakati wakipanga kumtafuta, Alex aliyekuwa karibu yao aliwaambia kwamba marehemu alikuwa amekwenda Minjingu na kuwa baada ya kupata taarifa hizo walisitisha kumtafuta hadi siku iliyofuata baada ya harufu kusikika chumbani kwa marehemu.
Shahidi wa nane ambaye ni shangazi wa marehemu, alishuhudia kuwa alitambua Alex na Kudura walikuwa wapenzi na alikuwa akiwasuluhisha kila walipotofautiana.
Katika utetezi wake, Alex alidai kumtambua Kudura kama jirani yake aliyekuwa mlevi na kukana kuwa na uhusiano naye wowote wa kimapenzi.
Hata hivyo kumbukumbu za Mahakama zinaonyesha kuwa alipohojiwa kwa kina, alikiri kwamba yeye na marehemu walikuwa wapenzi na alikuwa akimwona mara kwa mara na kukataa Septemba 15, 2020 kuongozana naye na kuwa siku hiyo alikuwa ziwani akivua samaki.
Alidai kutowaeleza shahidi wa nne na tano kuwa marehemu alikuwa ameenda Minjingu huku akikiri kwamba alikuwa akigombana na marehemu na shahidi wa nane alikuwa akiwapatanisha.
Kutokana na ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama iliridhika ukweli kwamba kifo cha marehemu hakikuwa cha kawaida ulithibitishwa zaidi ya shaka inayoeleweka na kumtia hatiani Alex kwa mauaji hayo na kumuhukumu adhabu ya kifo kutokana na ushahidi wa kimazingira.
Katika rufaa hiyo mrufani alikuwa na sababu nane ikiwemo ushahidi wa kimazingira haukumtaja mrufani kama mtu aliyemuua marehemu, hatia hiyo ilitokana na ushahidi wa kutiliwa shaka, kesi dhidi yake haikuthibitishwa bila shaka yoyote.
Baada ya kusikia mawasilisho yaliyotolewa na pande zote mbili, majaji hao walieleza kuwa uamuzi wao unapitia masuala matatu ambayo ni kama kifo hicho hakikuwa cha kawaida, ushahidi wa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu na uthabiti na uaminifu wa ushahidi wa kimazingira.
Jaji amesema baada ya kupitia hoja zote na mwenendo wa kesi ya msingi, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulitimiza wajibu wake wa kisheria wa ushahidi kwa kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba kifo cha marehemu hakikuwa cha asili.
Aidha mahakama ilijiridhisha kuwa ushahidi wa kimazingira uliomuhusisha mrufani na mauaji hayo uliweza kuthibitishwa na kuwa mrufani hakupinga ushahidi wa mashahidi walioeleza hayo.
“Kwa upande wetu, baada ya kutathmini ushahidi wa shahidi wa nne na ushahidi wote uliorekodiwa, tunakubaliana kuwa hauwezi kutiliwa shaka. Ushahidi wake ulikuwa thabiti na wa kutegemewa.” “Kulingana na yaliyotangulia, tunaridhika kwamba mazingira yaliyotajwa yanaashiria hatia ya mrufani, mazingira hayo hayaendani tu na hatia ya mrufani lakini pia hayana maelezo mengine yoyote zaidi ya hatia ya mrufani.
“Mrufani akiwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu na kushindwa kwake kutoa maelezo kuhusu kilichotokea na jinsi alivyoachana na marehemu na kuendelea na uongo wake kwa shahidi wa nne na tano, kwamba marehemu alikuwa amekwenda Minjingu, hayaachi shaka yoyote kwamba ni yeye ndiye aliyemuua.”
“Kwa yote yaliyosemwa na tumeridhika kwamba kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila shaka yoyote na hivyo ni sahihi alichokuhukumiwa. Kwa hivyo, rufaa hii inatupiliwa mbali,” walihitimisha majaji hao.
