Bei ya mafuta yaibua vyama vya wafanyakazi

Dar es Salaam. Wakati gharama za usafiri na vyakula zikiendelea kupanda kufuatia ongezeko la bei ya mafuta, vyama vya wafanyakazi vimeiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza makali ya maisha yanayowaathiri wafanyakazi.

Kupanda kwa bei ya mafuta kumetokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati kufuatia kufungwa kwa mlango wa bahari wa Mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia, hali inayosababisha uhaba na kupanda kwa bei kwa haraka.

Vyama hivyo vinasema licha ya kupanda kwa gharama za maisha, mishahara ya wafanyakazi imeendelea kubaki palepale, hali inayosababisha mzigo mkubwa kwao.

Athari za kupanda kwa bei ya mafuta tayari zimeanza kuonekana katika sekta ya usafiri, mfano kwa watumiaji wa bajaji jijini Dar es Salaam, nauli imeongezeka kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500, huku safari zilizokuwa zikigharimu Sh2,000 sasa zikifikia Sh2,500.

Aidha, gharama za kusafirisha mifugo kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam zimeongezeka kutoka Sh1.3 milioni hadi Sh1.5 milioni. Ongezeko hilo limesababisha bei ya nyama mabuchani kupanda kutoka Sh11,000 hadi Sh13,000 kwa kilo.

Akizungumzia hali hiyo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya, amesema athari za kupanda kwa bei ya mafuta ni za dunia nzima, si Tanzania pekee.

Amesema mafuta yanaathiri sekta nyingi ikiwemo chakula na usafiri, ingawa katika sekta ya afya athari hazionekani kwa kiwango kikubwa kutokana na huduma zinazotolewa na Serikali.

“Sisi wafanyakazi tunalia kama wanavyolia wananchi wengine. Tunaiomba Serikali iangalie bei ya mafuta kwa sababu athari ni kubwa. Ikiwezekana, itumie akiba ya mafuta ili kupunguza makali ya hali hii,” amesema.

Pia ameishauri Serikali kudhibiti wafanyabiashara ili wauze mafuta kwa kuzingatia bei waliyonunulia, badala ya kutumia mpya wakati bado wana akiba ya mafuta ya zamani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tarewu), Michael Marere, amesema kupanda kwa bei ya mafuta kumeathiri huduma nyingi huku mishahara ya wafanyakazi ikibaki bila mabadiliko.

“Katika kipindi hiki, waajiri wanapaswa kuwasaidia wafanyakazi kupunguza gharama za maisha. Kwa mfano, kutumia usafiri wa pamoja au kuwa na huduma za chakula ofisini ili kupunguza gharama,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Utafiti, Taaluma na Mashirika (Raawu) Taifa, Jane Mihanji, amesema kupanda kwa bei ya mafuta kunatokana na hali ya kimataifa, lakini bado wafanyakazi wanaumia zaidi.

“Wafanyakazi ndio walipakodi wakubwa kwa sababu kodi hukatwa moja kwa moja kwenye mishahara yao. Tunaiomba Serikali itafute namna ya kupunguza makali ya hali hii,” amesema.

Ameongeza kuwa hata watumiaji wa gesi katika vyombo vya moto wameathirika, huku gharama za vyakula na huduma nyingine zikizidi kupanda.

Pia ametoa wito kwa mataifa yenye migogoro kurejea kwenye amani, akisema migogoro hiyo inaathiri hata nchi zisizohusika moja kwa moja.

“Niwaombe wafanyakazi waendelee kuwa watulivu wakati tukisubiri hatua za Serikali,” amesema.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo Tanzania (TPAWU), John Vaaye, amesema ongezeko la bei ya mafuta ni pigo kubwa hasa kwa wafanyakazi wa sekta binafsi vijijini.

“Tunapitia maumivu makali kutokana na kupanda kwa gharama za maisha huku vipato vyetu vikiwa vidogo. Serikali inapaswa kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu,” amesema.

Mwanzoni mwa Aprili 2026, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bajeti ya mwaka 2026/2027 bungeni Dodoma, aligusia suala la kupanda kwa bei ya mafuta na kusema Serikali inaendelea kulifanyia kazi.

“Tumeona bei zimeanza kupanda. Tutahakikisha tunatafuta njia bora ya kukabiliana na hali hii ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nafuu na kudhibiti ongezeko la gharama za maisha,” amesema.

Aprili 7, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dk James Mataragio, alisema taarifa rasmi itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazohitajika.