Dar es Salaam. Licha ya juhudi mbalimbali za Serikali kuboresha afya ya uzazi, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, imebaini udhaifu katika mifumo ya takwimu, huduma na rufaa unaochangia kuendelea kwa vifo vya wajawazito vinavyoweza kuzuilika.
Changamoto za kumbukumbu zimeonekana zaidi katika hospitali za rufaa za mikoa, ambapo ni asilimia 48 tu ya vifo 344 vilivyoripotiwa kati ya mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2024/25, vilikuwa na taarifa kamili.
Amesema tofauti kati ya rejesta za vituo na mfumo wa kidijitali wa DHIS2 zimeendelea kudhoofisha uaminifu wa takwimu hizo.
CAG Kichere amebainisha hayo katika ripoti Ukaguzi Mkuu wa Afya ya Uzazi kwa mwaka 2024/2025 iliyowasilishwa bungeni Aprili 10, 2026.
Ripoti hiyo inasema vifo vya uzazi vimepungua kwa asilimia 14.1 kutoka 1,744 mwaka 2018 hadi 1,498 mwaka 2023, ingawa kasi hiyo ni ndogo kulinganisha na lengo la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Endelevu linalotaka nchi kufikia vifo 70 tu kwa kila vizazi hai 100,000, ifikapo mwaka 2030.
Aidha, idadi ya vifo imebainika kubaki ileile tangu mwaka 2023, ambapo jumla ya vifo 346 viliripotiwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Vifo hivyo viliathiri zaidi wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 34, na kwa kiasi kikubwa vilisababishwa na hali zinazoweza kuzuilika kama vile kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua na kifafa cha mimba.
“Ukaguzi umebaini kuwa mfumo wa ufuatiliaji wa vifo vya mama na mtoto mchanga (MPDSR) haujatumika ipasavyo, jambo linalodhoofisha matumizi ya takwimu katika kupanga mikakati ya kuokoa maisha.
“Ingawa karibu vifo vyote huripotiwa, ni asilimia 65 pekee vinavyofanyiwa mapitio, huku karibu nusu ya matukio yakikosa uchambuzi kabisa,” amebainisha CAG.
Aidha, hata katika matukio yanayopitiwa, utekelezaji wa taarifa zake ni hafifu. Takribani asilimia 45 ya matukio hayana mipango ya utekelezaji, na kati ya mipango iliyopo, asilimia 62 haina ushahidi wa kufuatiliwa.
CAG ameonya kuwa hali hiyo inaacha pengo kubwa kati ya takwimu na hatua za vitendo.
Ukaguzi huo pia umebaini Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) hazijatumia kikamilifu takwimu zilizokusanywa kubuni hatua za kuzuia vifo.
“Matokeo yake, vifo vinavyoweza kuzuilika vinaendelea kujirudia. Katika vituo vilivyotembelewa, vifo 198 vilibainika kuwa vingeweza kuepukika, vingi vikisababishwa na kutokwa damu nyingi na shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito,” amesema.
CAG ametaja sababu za mapungufu hayo ni pamoja na uhaba wa watumishi, mzigo mkubwa wa kazi, mafunzo duni, kutokuwepo kwa mifumo jumuishi ya taarifa na utegemezi wa kumbukumbu za karatasi.
Pia, anasema kamati za mapitio hazifanyi kazi ipasavyo na vikao vingi hufanyika nje ya muda uliopangwa au kutofanyika kabisa.
Katika upande wa huduma, ripoti ya ukaguzi wa ufanisi imeonyesha upungufu mkubwa wa wataalamu wenye ujuzi wa kuhudumia uzazi, hali inayochangia matumizi madogo ya huduma za kliniki za wajawazito na za baada ya kujifungua.
“Hali hii imeongeza uwezekano wa wanawake kujifungulia majumbani, hasa katika maeneo ya vijijini,” amesema.
“Mfumo wa rufaa pia umeelezwa kuwa dhaifu. Licha ya asilimia 96.7 ya rufaa kuanzishwa na kukamilika, bado asilimia 3.3 hazifuatiliwi, jambo linaloonyesha upungufu katika uratibu.
“Changamoto kubwa ni upungufu wa magari ya wagonjwa. Kati ya magari 1,245 yanayohitajika, ni 607 tu yanapatikana, sawa na asilimia 49,” imeeleza ripoti hiyo.
CAG amesema magari mengi yaliyopo hayana vifaa muhimu na yamejikita zaidi mijini, huku maeneo ya visiwa yakikabiliwa na hali mbaya zaidi ambako baadhi ya boti za wagonjwa hazifanyi kazi kabisa.
Aidha, madereva wengi hawajapatiwa mafunzo ya huduma za dharura kama na matumizi ya vifaa vya kuokoa maisha.
Kutokana na hali hiyo, CAG anasema wanawake wengi hukumbwa na ucheleweshaji katika kufikishwa kwenye huduma za dharura, jambo linaloongeza hatari ya madhara kwa mama na mtoto.
Kwa ujumla, ripoti inahitimisha kuwa Wizara ya Afya na Tamisemi hazijafanikiwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya ya uzazi.
“Upungufu katika huduma za dharura za uzazi, uhaba wa watumishi, udhaifu wa mifumo ya takwimu na rufaa, pamoja na utegemezi mkubwa wa wafadhili, vimeendelea kudhoofisha juhudi za kitaifa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, CAG amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kitaifa wa kidijitali utakaorahisisha ukusanyaji, uhifadhi na ufuatiliaji wa taarifa, pamoja na utekelezaji wa programu za kidijitali katika ngazi za mikoa.
Pia, Serikali imeshauriwa kuongeza magari ya wagonjwa na usafiri majini, na kuimarisha mafunzo ya huduma za dharura kwa watoa huduma za afya, vinginevyo maisha ya akina mama yataendelea kupotea kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.
