CAG abaini uhaba wa madaktari wa mazoezi, wauguzi MOI

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, Charles Kichere imebaini kuwepo kwa uhaba mkubwa wa madaktari wa mazoezi ya viungo na wauguzi katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), hali inayochangia kuchelewa kwa uponyaji wa wagonjwa na kuathiri ubora wa huduma za afya.

Hayo yamebainishwa katika ripoti kuu ya mwaka ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyokabidhiwa katika Bunge la Tanzania Ijumaa ya Aprili 2026.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wagonjwa kadhaa katika wodi za MOI hawapati huduma stahiki kwa wakati kutokana na uhaba wa watumishi na mzigo mkubwa wa kazi, jambo linalotishia kufikiwa kwa malengo ya kupunguza muda wa kulazwa hospitalini kutoka siku 14 hadi saba ifikapo Juni 2026.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, kwa mujibu wa sehemu ya 6.2 ya Mwongozo wa Utendaji wa MOI wa mwaka 2023, madaktari wa mazoezi wanatakiwa kutembelea wagonjwa mara kwa mara wodini ili kufuatilia maendeleo yao.

Hata hivyo, ukaguzi ulibaini kuwa wagonjwa 38 hawakutembelewa kama ilivyopangwa, kutokana na uhaba wa madaktari hao pamoja na changamoto za ratiba.

CAG anabainisha kuwa MOI inahitaji angalau madaktari wa mazoezi 12 zaidi ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

“Kutotembelewa kwa wagonjwa kwa wakati kunapunguza kasi ya uponyaji, hali inayosababisha wagonjwa kukaa muda mrefu hospitalini na hivyo kupunguza nafasi kwa wagonjwa wapya wanaohitaji huduma,” imeeleza ripoti hiyo.

Katika eneo la uuguzi, ripoti hiyo inaonyesha kuwa kuna pengo kubwa kati ya uwiano unaotakiwa na hali halisi. Mwongozo wa MOI unapendekeza muuguzi mmoja kwa wagonjwa watatu, lakini hali ilivyo ni muuguzi mmoja kuhudumia wagonjwa sita hadi wanane.

CAG anaeleza kuwa hali hiyo inasababisha muda mdogo wa huduma kwa kila mgonjwa na kuongeza uchovu kwa wauguzi, jambo linalopunguza ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa.

Aidha, mzigo mkubwa wa kazi unatajwa kuongeza hatari ya makosa ya kibinadamu katika utoaji wa huduma za afya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mwaka wa fedha 2024/25, MOI iliidhinisha ajira ya watumishi wapya 223, lakini ilipata kibali cha nafasi 91 pekee. Hadi sasa, watumishi 68 wameajiriwa na usaili umekamilika kwa nafasi 23 zilizosalia.

Kutokana na changamoto hizo, CAG ametoa mapendekezo mahsusi kwa MOI ili kuboresha utoaji wa huduma.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuimarisha usimamizi wa ndani kwa kuhakikisha tathmini ya kila siku inafanyika ili kuthibitisha kuwa madaktari wa mazoezi wanatembelea wagonjwa wodini kwa mujibu wa ratiba, huku ushahidi wa utekelezaji huo ukiwekwa wazi.

“Ninapendekeza kuongezwa kwa idadi ya madaktari wa mazoezi kwa kuharakisha ajira mpya ili kupunguza mzigo wa kazi uliopo kwa sasa.

“Pia, ninasisitiza umuhimu wa MOI kuendelea kufuatilia vibali vya ajira kwa wauguzi ili kufikia uwiano unaopendekezwa wa muuguzi mmoja kwa wagonjwa watatu,” amependekeza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya MOI, Dk Mpoki Ulisubisya amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na jitihada zinazofanywa na hospitali na Serikali kupitia Wizara ya Afya.

“Wataalamu tulionao wachache wanafanya kila wanachoweza kuhakikisha wagonjwa wote wanahudumiwa, lakini pia wizara wanalishughulikia. Tulichofanya ni kuweka ratiba kuondoa ombwe lililopo. Tunatumia waliopo na kusomesha wataalamu zaidi,” amesema Dk Ulisubisya.

Pia, baadhi ya wagonjwa waliowahi kulazwa hospitalini hapo baada ya kupata ajali, wanasema walitumia muda mrefu wodini wakiwa wamelazwa.

Asha Ally, 41 aliyelazwa MOI baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu, anasema alipata changamoto ya kuchelewa kuanza huduma za mazoezi ya viungo kutokana na ukosefu wa ufuatiliaji wa karibu.

“Nilikaa zaidi ya wiki mbili bila kuanza mazoezi kama ilivyopangwa. Wakati mwingine daktari wa mazoezi hakuwepo wodini kwa wakati, hali iliyochelewesha kuanza kutembea tena,” amesimulia.

Asha amesema wauguzi walijitahidi, lakini walikuwa wachache na wenye mzigo mkubwa wa kazi, jambo lililoathiri muda na ubora wa huduma aliyopata.

Kwa upande wake, John Mwakalonge aliyelazwa baada ya ajali ya pikipiki, amesema huduma za ufuatiliaji zilikuwa hafifu.

“Wauguzi walikuwa wachache na wakati mwingine ilibidi usubiri muda mrefu kupata msaada. Hata daktari wa mazoezi hakufika mara kwa mara,” amesema.

Ripoti hiyo inaonya kuwa bila kuchukuliwa hatua za haraka, juhudi za kuboresha ubora wa huduma na kupunguza muda wa kulazwa hospitalini zinaweza kutofikiwa, hali itakayoendelea kuathiri wagonjwa na mfumo mzima wa huduma za afya nchini.