Dar es Salaam. Licha ya kuongezeka kwa mahitaji ya barabara nchini, Serikali kwa miaka minne mfululizo imetekeleza kwa wastani wa asilimia 50 tu maboresho ya barabara zilizopangwa kati ya mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2024/25.
Hiyo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ya mwaka wa fedha 2024/25, iliyochambua usimamizi wa mchakato wa mipango ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Aidha, amesema Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura) zenye jukumu ya kuhudumia barabara zake zimekuwa zikitengezwa bajeti kiduchu na hivyo kushindwa kufikia malengo huku fedha nyingine zilizotengwa zikiwa hazitolewi kikamilifu.
Vilevile, amebainisha kuwa Wizara ya Ujenzi pamoja na Tamisemi hazijaandaa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Miundombinu ya Barabara, ambao ungeongoza maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
CAG Kichere amebainisha dosari hizo, siku chache baada ya wabunge kupaza sauti kwa Serikali, wakiitaka kutoa kipaumbele kwa suala la uboreshaji wa barabara hususan zinazosimamiwa na Tarura, ili kuleta unafuu kwa wananchi.
Wabunge hao wametoa kilio hicho wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilisha bungeni Aprili mosi.
Sehemu kubwa ya michango ya wabunge kwenye mjadala huo utakaohitimishwa Aprili 14, 2026 wanataka ubovu wa barabara uchukuliwe kama jambo la dharura kwa kuwa wananchi wao wanateseka, hususan nyakati za masika.
Wabunge waliitaka Serikali kuipata Tarura fedha za kutosha ili kukarabati na kuzitengeneza barabara nyingi zilizoharibika.
Jitihada za kupata viongozi wa Tamisemi na Wizara ya Ujenzi kuelezea dosari ambazo CAG amezibainisha hizo na hawakupatikana.
Hata hivyo, moja ya hoja ambayo itakuwa inasubiriwa na wabunge kujibiwa wakati wa kuhitimishwa kwa mjadala wa hotuba ya waziri mkuu, ni suala hili la barabara kwa kuwa limezungumzwa na wabunge wengi.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG iliyowasilishwa bungeni Aprili 10, hali hiyo ya kupunguza bajeti inasababisha utekelezaji hafifu wa mipango ya kuboresha miundombinu ya barabara.
Amesema ukaguzi umeonyesha malengo ya kila mwaka ya uboreshaji wa barabara yamekuwa yakipungua badala ya kuongezeka kutoka kilomita 1,227 mwaka 2021/22 hadi kilomita 1,023 mwaka 2024/25.
“Utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo kuboresha barabara hadi kiwango cha lami na za changarawe, ulikuwa na tofauti kubwa kati ya miaka, hali iliyoathiri kasi ya maendeleo ya sekta hiyo.
“Kwa maboresho ya barabara za changarawe yalitekelezwa kwa viwango vinavyokadiriwa kati ya asilimia 39 hadi 69, wakati yale ya barabara za lami yalikuwa kati ya asilimia 45 hadi 65.
Hata hivyo, ni mwaka mmoja pekee wa fedha 2024/25 ambapo malengo ya uboreshaji wa barabara za lami yalifikiwa kikamilifu,” imesema ripoti hiyo.
CAG ametaja sababu kadhaa zilizochangia hali hiyo, ni pamoja na ukosefu wa upangaji madhubuti wa vipaumbele katika mipango ya maboresho ya miundombinu ya barabara pamoja na uhamasishaji duni wa rasilimali fedha.
Amesema hali hiyo imesababisha kucheleweshwa kwa utekelezaji wa miradi mingi ya barabara, na hivyo kuathiri huduma za usafiri kwa wananchi.
Kuhusu fedha zilizotengwa kutokutolewa amesema nalo ni tatizo ambalo limekuwa linaongezeka kila mwaka.
“Nilibaini kuwa kutotolewa kwa fedha kikamilifu zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya barabara kumesababisha ongezeko la malimbikizo ya madai ya malipo ambayo hayajalipwa yanayohusiana na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Amesema kufikia Juni kwa mwaka 2021/22, malipo yaliyokuwa yakidaiwa kwa ajili miradi ya uboreshaji wa barabara chini ya Wakala wa Barabara nchini yalikuwa Sh0.633 trilioni, ambapo yaliongezeka hadi Sh0.701 trilioni kwa mwaka 2022/23, kisha Sh1.295 trilioni na hatimaye kufikia Sh1.221 trilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24 na 2024/25 mtawalia.
Anasema ucheleweshaji wa utoaji wa fedha pia ulisababisha
Serikali kuingia gharama za ziada kutokana na tozo za riba kwenye malipo yaliyochelewa au tofauti za viwango vya kubadilishia fedha za kigeni, kwa kuwa malipo yalifanyika kwa fedha za kigeni.
“Kwa mfano, wakati wa ukaguzi huu, miradi minne kutoka mikoa iliyotembelewa ilikuwa na madai ya riba ya Sh5.6 bilioni kutokana na kuchelewa kwa malipo.
Miradi hiyo ilikuwa ni barabara ya Nachingwea-Nanganga na Chunya-Makongorosi, ambazo zilipata tozo za riba za Sh2.984 bilioni na Sh824.86 milioni mtawalia, na barabara ya Nsalaga-Ifisi jijini Mbeya na barabara ya mzunguko ya Dodoma awamu ya kwanza ambazo zilirundika tozo za riba ya Sh764.51 milioni na Sh1.03 bilioni mtawalia.
Aidha, ripoti imebainisha Wizara ya Ujenzi pamoja na Tamisemi hazijaandaa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa miundombinu ya barabara, ambao ungeongoza maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
“Kutokuwepo kwa mpango huo kumetajwa kuwa chanzo cha ukosefu wa mwelekeo wa pamoja katika kupanga vipaumbele na kuvutia uwekezaji katika sekta ya barabara,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Katika suala la fedha, ripoti hiyo imeonyesha ugawaji na uhamasishaji wa rasilimali haukuendana na mahitaji halisi ya maboresho ya barabara.
“Kwa mfano, fedha zilizotengwa kwa barabara za mikoa zilipungua kutoka Sh94.64 bilioni mwaka 2021/22 hadi Sh87.27 bilioni mwaka 2023/24 na kubaki katika kiwango hicho mwaka 2024/25.
“Kwa upande wa barabara za wilaya zinazohudumiwa na Tarura, bajeti ilishuka kutoka Sh716.8 bilioni mwaka 2021/22 hadi Sh704.9 bilioni mwaka 2022/23, na kupungua zaidi hadi Sh704.7 bilioni mwaka 2023/24. Kiwango hicho kibaki bila mabadiliko mwaka 2024/25,” imeeleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa CAG, mwenendo huo unadhoofisha uwezo wa taasisi husika kutekeleza miradi iliyopangwa kwa wakati na kwa ufanisi.
CAG pia ameeleza matumizi ya ukomo wa bajeti badala ya kupanga vipaumbele kulingana na mahitaji halisi yamechangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo, na kusababisha baadhi ya miradi muhimu kutotekelezwa huku rasilimali chache zikielekezwa kwenye maeneo yasiyo ya kipaumbele.
Kwa upande wa upangaji wa miradi, ripoti imebaini Wizara ya Ujenzi na Tamisemi hazijatoa kipaumbele kinachostahili kwa maboresho ya miundombinu ya barabara kulingana na mahitaji yaliyopo.
Aidha, CAG ameukosoa Mpango Mkakati wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wa miaka ya 2021/22 hadi 2025/26 kwa kukosa mfumo wa wazi wa kupanga vipaumbele.
“Katika mpango huo, tafiti 132 za upembuzi yakinifu pamoja na miradi 81 ya kuboresha barabara za mikoa zenye urefu wa kilomita 9,346 zilipangwa bila kufanyiwa tathmini ya kina inayozingatia hali halisi ya barabara, umuhimu wake kiuchumi au athari zake kwa jamii.
Hata hivyo, kwa upande wa Tarura, licha ya kuwa na vigezo vya kupanga vipaumbele vinavyozingatia hali ya barabara, msongamano wa magari na mahitaji ya kijamii na kiuchumi, vigezo hivyo havikutumika ipasavyo katika uteuzi wa miradi.
CAG ameonya hali hiyo inaweza kusababisha matumizi mabaya ya rasilimali na kusababisha miradi yenye umuhimu mdogo kupewa kipaumbele, huku ile ya dharura ikipuuzwa, jambo linalodhoofisha maendeleo ya mtandao wa barabara nchini.
Vilevile, ukaguzi umebaini kuwepo kwa udhaifu katika uratibu wa wadau mbalimbali katika mchakato wa kupanga na kuboresha miundombinu ya barabara.
Kwenye hili imeelezwa kuwa hakuna mfumo madhubuti wa kuwashirikisha wadau muhimu kama Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango katika hatua za kupanga vipaumbele na kutafuta rasilimali.
Kutokana na hali hiyo, CAG ametoa mapendekezo kadhaa ikiwemo kuboresha upangaji wa vipaumbele, kuandaa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Barabara, pamoja na kuongeza uhamasishaji wa rasilimali fedha.
Pia amesisitiza umuhimu wa kufanya makadirio sahihi ya gharama na kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati ili kufanikisha miradi ya maboresho ya barabara.
Amesema utekelezaji wa mapendekezo hayo utasaidia kuimarisha sekta ya usafiri na kuchangia kufikia malengo ya maendeleo endelevu, hususan kuhakikisha upatikanaji wa mifumo ya usafiri iliyo salama, nafuu na endelevu kwa wananchi.
