Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza kushangazwa na kile kilichokiita kutochukuliwa kwa hatua za haraka na mamlaka husika katika kudhibiti kupanda kwa bei ya mafuta, huku kikisema wanaoumia zaidi ni wananchi.
Chama hicho kimesema suluhisho ni kuondoa kodi na tozo zilizopo kwenye mafuta, huku kikisisitiza kuwa suluhisho si kulalamika au kupunguza magari katika misafara ya viongozi.
Chadema inasema hayo ikiwa ni siku 12 zimepita tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la bei za mafuta, ambapo kwa Jiji la Dar es Salaam, bei ya petroli imepanda kutoka Sh2,864 Machi hadi kufikia Sh3,820 Aprili, 2026.
Ongezeko hilo linatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya sintofahamu katika soko la kimataifa la mafuta, hususan kutokana na mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati unaohusisha Marekani, Israel na Iran.
Akizungumza leo, Aprili 12, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Amani Golugwa, ameonesha wasiwasi kuhusu kutochukuliwa kwa hatua au juhudi za kupunguza makali yanayosababishwa na kupanda kwa bei hizo.
“Tunaona mamlaka zinachelewa kuchukua hatua kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta na Chadema tulishazungumza awali, lakini kauli zinazotolewa hazioneshi watu wanaotafuta suluhisho bali kujaribu kujilinda kisiasa mbele ya hasira ya umma,” amesema.
Golugwa amesema Chadema imeshatoa hoja na mwelekeo wa suluhisho katika changamoto hiyo, lakini cha ajabu wenye mamlaka wanatoa kauli zisizo na mwelekeo wa kutafuta suluhisho.
“Soko la dunia si chanzo pekee, bali inaonesha wazi namna mfumo wa ndani unavyoshindwa kubeba mitikisiko ya nje kwa ufanisi. Katika mazingira ya dharura kama haya, ni dhahiri kuna kukosekana kwa uwajibikaji,” amesema Golugwa.
Amesema Chadema ilishatoa pendekezo na suluhisho la mazingira ya dharura kwamba tozo iliyoongezeka kutoka bei ya awali, kwa mfano Dar es Salaam, imepanda kwa takriban Sh1,000, na kwamba kutokana na kuwepo kwa akiba ya mafuta ya miezi mitatu, ambayo haijaathirika na tatizo hilo, inaashiria kutojali wananchi hata katika mazingira kama haya.
“Tuliambiwa kuna akiba ya miezi mitatu. Kitaalamu lengo lake ni kupunguza au kuchelewesha mshtuko wa bei kwa mlaji wa mwisho ikiwa bei katika soko la dunia zitapanda ghafla kama ilivyo sasa. Sasa ile akiba hutumika kuingilia soko kupunguza utegemezi wa uagizaji wa gharama kubwa kwa muda mfupi, hivyo kulinda uchumi wa ndani, lakini tunaona imekuwa kinyume,” amesema.
Golugwa amesema akiba iliyotangazwa ilipaswa itumike katika kipindi hiki, hali ambayo ingepunguza makali wakati wa mshtuko wa bei.
Akifafanua zaidi, Golugwa amesema kuna msururu wa kodi na tozo zinazomlemea mlaji ambazo ukijumlisha zinafikia 18 kwenye lita moja ya mafuta.
“Hili ongezeko la Sh1,000 liondolewe na irudi bei ya awali, kwa kuwa katika bei hiyo hizo kodi zilishakokotolewa. Tunapaswa tufaidike na akiba iliyopo ambayo mamlaka ilitangaza,” amesema.
Golugwa amesema viongozi wana wajibu wa kulinda wananchi kupitia manufaa ya akiba hiyo ya miezi mitatu, kwa kuwa wanaelewa hali ya wananchi na nguvu zao za kiuchumi.
