Klabu ya Gymkhana, Mwananchi wapanda miti 600 kwa lengo la kuboresha mandhari

Klabu ya michezo ya Dar es Salaam Gymkhana Club, kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imepiga hatua muhimu katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti 600, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulifanya jiji kuwa safi, lenye mvuto na rafiki kwa mazingira.

Zoezi hilo lililofanyika Aprili 11, 2026, liliwakutanisha wanachama wa klabu hiyo pamoja na wafanyakazi wa MCL.

Meneja Mkuu wa klabu hiyo, Lilian Msangi, alisema hatua hiyo inalenga kuboresha mandhari ya klabu na kuifanya kuwa kivutio zaidi kwa wanachama na wageni.

Alibainisha kuwa upandaji wa miti utakuwa ni utaratibu wa kudumu unaotekelezwa kila mwaka kama sehemu ya utamaduni wa klabu katika kulinda mazingira.

“Tunawashukuru sana Mwananchi Communications Limited kwa ushirikiano wao mkubwa. Hili ni jambo la kujivunia, na pia tunathamini mchango wa wanachama na wafanyakazi wote walioshiriki,” alisema Msangi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya klabu hiyo, Francis Kiwanga, alisema klabu hiyo yenye historia ya zaidi ya miaka 100 inaendelea kuboresha miundombinu na mazingira yake ili kuendana na mahitaji ya kisasa. Alieleza kuwa upandaji wa miti una manufaa makubwa, ikiwemo kuboresha ubora wa hewa, kupunguza joto, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda viumbe hai.

Aliongeza kuwa miti pia husaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza hewa ya ukaa, hivyo kuifanya klabu kuwa sehemu salama na yenye afya kwa watumiaji wake.

Naye Meneja Masoko wa MCL, Edson Sosten, alisema kampuni hiyo inajivunia kushiriki katika zoezi hilo, akisisitiza kuwa linaendana na dhamira ya taasisi hiyo ya “Kuliwezesha Taifa.”

“Sisi si tu tunatoa taarifa na kuelimisha umma, bali pia tunawajibika kwa mazingira tunayoyahudumia. Kwa kuwa kazi yetu inategemea sana matumizi ya karatasi, ni wajibu wetu kurejesha kwa mazingira sehemu ya tunachotumia,” alisema Sosten.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo unaonesha wazi kuwa uwezeshaji wa kweli hauishii kwenye maudhui pekee, bali unahitaji vitendo vinavyoleta mabadiliko chanya kwa jamii.

Kupitia mpango huo, MCL imeahidi kuendelea kuhimiza matumizi ya mbinu endelevu, kupunguza athari za kimazingira na kutumia majukwaa yake kuhamasisha jamii kushiriki katika kulinda mazingira.

“Kwa sababu kuliwezesha taifa pia kunamaanisha kulilinda kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisisitiza Sosten.