KOCHA wa Simba, Steve Barker, anakabiliwa na kibarua kingine kigumu leo Jumapili, wakati kikosi hicho kitakapokuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, kucheza dhidi ya Dodoma Jiji ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 16 bora.
Barker anakabiliwa na kibarua hicho, baada ya kushuhudiwa mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu akishindwa kupata ushindi, kufuatia suluhu ya 0-0 dhidi ya Azam, Aprili 5, 2026, kisha matokeo kama hayo mbele ya TRA United, Aprili 9, 2026.
Katika michuano ya CRDB msimu huu, Simba ilianza hatua ya 64 bora kwa kuichapa Greenland ya Kagera mabao 3-0, kisha 32 bora ikaichapa B19 FC mabao 2-0, ikihitaji kutwaa ubingwa huo baada ya kuuchukua mara ya mwisho msimu wa 2020-2021.
Kwa upande wa kikosi cha Dodoma Jiji, kilianza safari ya matumaini kwa kuichapa Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro mabao 3-1 katika hatua ya 64 bora, kisha ikafuzu 32 bora na kuitoa African Sports ya Tanga kwa mabao 2-0.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ni katika mechi iliyopigwa Februari 25, 2026, zilipotoka suluhu (0-0) ikiwa ni sare ya kwanza kwa Dodoma Jiji dhidi ya Simba, tangu ilipoanza kucheza Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2020-2021.
Mechi nyingine ya michuano hiyo hatua ya 16 bora leo Jumapili itapigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Airtel uliopo Singida, ambapo wenyeji Singida Black Stars, watakuwa na kibarua cha kuikaribisha Mbeya City.
Hatua ya 64 bora, Singida ilianza michuano hiyo kwa kuitoa Copco ya jijini Mwanza kwa kuichapa mabao 3-1, kisha 32 bora ikaitoa Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship kwa kuifunga pia mabao 3-1.
Singida iliyonolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Muhibu Kanu kwa kushirikiana na benchi jipya la ufundi, chini ya Meneja Mkuu wa timu hiyo, Mkongomani Papy Kimoto na Kocha Msaidizi, Kapiten Ngoyi Dora, wamebeba matumaini makubwa ya kikosi hicho.
Timu hiyo ilivunja benchi la ufundi lililokuwa linaongozwa na Mkenya, David Ouma na Meneja Mkuu wa kikosi hicho, Mtunisia Othmen Najjar, Aprili 5, 2026, baada ya mwenendo mbaya katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026.
Kwa upande wa Mbeya City, ilianza hatua ya 64 bora kwa kupata ushindi wa bure wa mabao 3-0, baada ya Biashara United inayojulikana kwa jina la utani la ‘Wanajeshi wa Mpakani’, kushindwa kutokea uwanjani bila ya kuweka sababu za msingi.
Katika hatua ya 32, timu hiyo inayonolewa na Kocha wa zamani wa Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Ihefu ambayo sasa ni Singida Black Stars, Mecky Maxime, ikakutana na Bandari Tanzania ya Mtwara inayoshiriki Ligi ya Championship na kuichapa mabao 3-0.
Mechi ya mwisho leo katika kuhitimisha raundi ya 16 bora, itapigwa saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo mabingwa wa michuano hii msimu wa 2018-2019, Azam wataikaribisha Fountain Gate.
Azam chini ya Kocha Mkongomani, Florent Ibenge, inaingia katika mechi hii ikiwa haina mwenendo mzuri kwa siku za karibuni, baada ya kutoka suluhu (0-0) mbili mfululizo kwenye ligi dhidi ya Simba, Aprili 5, 2026 na Mbeya City, Aprili 9, 2026.
Mbali na mwenendo huo usioridhisha kwa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara, hata kwenye michuano ya CRDB inasuasua licha ya kupenya hadi 16 bora, ambapo ilianza kwa kuifunga Endument FC ya Kilimanjaro bao 1-0, hatua ya 64 bora, kisha 32 bora ikaifunga Mbeya Kwanza pia bao 1-0.
Kwa upande wa Fountain Gate inayoingia katika mechi hiyo ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya Fredy Felix ‘Minziro’, ilianza hatua ya 64 bora kwa kuichapa Mapinduzi ya Mwanza bao 1-0, kisha 32 bora ikaifunga Gunners ya Dodoma mabao 2-1.
Mechi hiyo ni ya kwanza kwa Minziro tangu atambulishwe kukiongoza kikosi hicho, baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Ismail ‘Laizer’, kusitishiwa mkataba wake kwa makubaliano ya pande zote mbili, Aprili 10, 2026.
