Dar es Salaam. Wanaoajiri wasaidizi wa kazi nchini wamekumbushwa kuzingatia kipengele cha umri kwani kumuajiri msaidizi wa kazi za ndani mwenye umri wa chini ya miaka 18 ni kosa kisheria na ni kitendo cha ukatili.
Hayo yamebainishwa jana Aprili 11, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa semina iliyowakutanisha wamiliki wa makazi yanayojishughulisha na malezi ya watoto, wasaidizi wa kazi za ndani pamoja na wadau wengine wa malezi.
Akizungumza katika semina hiyo Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Leah Ezekiel amesisitiza kuwa wanaofanya hivyo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni ukatili wa kijinsia.
“Ninawasihi wanaoajiri watoto wa chini ya miaka 18 kufanya kazi za ndani waache mara moja kwani sharia ya nchi inapinga vikali lakini pia kuna madhara ya kimwili na kisaikolojia kwa mtoto huyo,”amesema.
Katika hatua nyingine ofisa huyo kutoka Kitengo cha Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe amesema ujio wa mafunzo kwa wasaidizi wa ndani kwa ngazi ya cheti na stashahada kutasaidia kukuza hadhi ya wasaidizi hao ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakidharauliwa na baadhi ya watu.
Pia amesema itasaidia wasaidizi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na nidhamu ya hali ya juu kutokana na mafunzo ambayo wanapewa.
“Niwasihi wasaidizi wa kazi za ndani kutumia fursa za mafunzo yanayohusiana na kazi hizo ili kuongeza ujuzi na kupata heshima katika jamii,”amesema.
Kauli ya Leah inaungwa mkono na Makamu Mkuu wa Chuo cha Padre Pio, Dk Yasin Mussa ambaye amesema kuanzishwa kwa mafunzo kwa wasaidizi wa majumbani kutaboresha zaidi namna wanavyotoa huduma
Anasema baadhi ya wahudumu na wasaidizi wa majumbani wamekuwa wakihudumia watu wa makundi maalum kama wazee, watoto na hata wagonjwa katika ngazi ya familia bila ya kuwa na utaalamu wa namna gani ya kuweza kuwahudumia kutokana na hali walizonazo au ugonjwa unaowasumbua, “Na kujikuta wakifanya yote hayo kwa kutumia tu uzoefu walionao.”
Washiri mbalimbali waliohudhuria wakati wa semina iliyowakutanisha wamiliki wa makazi yanayojishughulisha na malezi ya watoto, wasaidizi wa kazi za ndani pamoja na wadau wengine wa malezi.
Dk Yassin amesema kuwa baadhi ya wahudumu hawana hata ujuzi wa kutoa huduma ya kwanza pindi ajali inapotokea nyumbani jambo ambalo si la kulifumbia macho.
Amesema mafunzo hayo wahudumu hao katika ngazi ya familia wanafundishwa mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kuwahudumia wagonjwa kulingana na ugonjwa husika, masuala ya lishe, utunzaji wa watoto kwa mujibu wa kanuni za afya, namna ya kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo wazee pamoja na wenye ulemavu na utoaji wa huduma ya kwanza.
Hiyo itawasaidia kutoa huduma bora zaidi kwa wale wanaowahudumia.
Hivyo aliwasisitiza waajiri kuwawezesha wasaidizi wao wa kazi za ndani kupata mafunzo hayo ambayo ni muhimu katika kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi.