Laizer aondoka Fountain Gate kwa amani

ALIYEKUWA Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema licha ya kuachana nayo hana kinyongo na jambo lolote, huku akisifia uhusiano mzuri aliokuwa nao kuanzia kwa wachezaji wa kikosi hicho na hadi viongozi kiujumla.

Uongozi wa timu hiyo, uliachana na Laizer Aprili 10, 2026, baada ya matokeo mabaya ya mechi za Ligi Kuu msimu wa 2025-2026, huku Fredy Felix ‘Minziro’, aliyetamba na Geita Gold, Pamba Jiji na Tanzania Prisons, akirithi mikoba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema ni muda sahihi kwake wa kuangalia fursa sehemu nyingine, ingawa hawezi kusema kwa sasa atakapokwenda, kwa sababu anahitaji kupumzika kwa muda, kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho wa majukumu mapya.

“Nashukuru kwa sapoti waliyonipa kwa kipindi chote nilichofanya nao kazi, makocha hatuna dhamana ndio maana leo unaweza ukawa sehemu hii na kesho ukaibukia kwingine, jambo la muhimu na la msingi nawatakia tu kila la heri,” amesema Laizer.

Laizer ambaye awali alikuwa kocha msaidizi, alipewa majukumu ya kocha mkuu kikosini hapo Septemba 28, 2025, ikiwa ni muda mfupi tangu, Kocha Mkuu, Denis Kitambi, aliyewahi kufundisha Simba, Namungo na Geita Gold, kuondoka.

Kitambi alijiunga na kikosi hicho kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mnigeria, Ortega Deniran, aliyeondoka mapema tu kabla ya msimu wa 2025-2026 kuanza na kumuachia kocha huyo ambaye hata hivyo, aliiongoza katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara.

Baada ya kuondoka Ortega, Kitambi aliiongoza Fountain Gate katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kupoteza zote, ambapo alichapwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, Septemba 18, 2025, kisha kuchapwa tena mabao 3-0 na Simba, Septemba 25, 2025.

Laizer ameiongoza Fountain Gate katika mechi 15 za Ligi Kuu Bara, kati ya hizo, alishinda nne, sare nne na kupoteza saba, ambapo timu hiyo ilifunga mabao nane na kuruhusu 18, akiiacha ikishika nafasi ya 14 na pointi 16.