Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini mamlaka za maji katika kanda nne nchini zimeshindwa kufikia viwango vinavyotakiwa vya upatikanaji wa maji.
Kulingana na CAG, Charles Kichere, upatikanaji wa maji kwenye mamlaka za maji nchini ni chini ya asilimia 35.
Hiyo ni kinyume na takwa la Mwongozo wa Tathmini ya Utendaji wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira wa mwaka 2022, unaoelekeza mamlaka za maji kufikia kiwango cha upatikanaji wa maji cha asilimia 84 kwa maeneo wanayohudumia.
Dosari hizo alizozibaini CAG zipo kwenye ripoti ya utendaji wa Mamlaka za Maji ya mwaka 2024/2025, ambapo katika ripoti hiyo kanda za Mashariki, Magharibi, Nyanda za Kusini na Kaskazini, upatikanaji wa maji kwa miaka minne tangu 2020/2021 hadi 2023/2024 ulikuwa chini ya kiwango.
Hali ya matumaini inaonekana pekee kwa mamlaka mbili za maji za Moshi (Kilimanjaro) na Mwanza, ambazo katika kanda zote zimefikia viwango vinavyohitajika kwa mwaka 2020/2021 kwa watu wanaowahudumia.
Mbali na mwaka huo, kuanzia 2021/2022 hadi 2023/2024 hakuna mamlaka yoyote ya maji iliyofikia viwango vinavyohitajika vya utoaji wa huduma ya maji.
Katika mamlaka hizo, CAG amebaini kuwa kiwango cha huduma ya maji ambacho mamlaka zimefanikiwa kutoa ni kati ya asilimia sifuri hadi 33.
Kwa kipindi cha 2020/2021, kiwango cha juu kilichorekodiwa cha utoaji wa huduma kwa Kanda ya Ziwa ni asilimia 33, huku kiwango cha chini kikibainika Kanda ya Mashariki kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
“Kanda ya Mashariki, Ziwa na Nyanda za Juu Kaskazini kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024 hazijafikia kiwango kinachohitajika cha utoaji wa huduma za maji,” ripoti hiyo imeeleza.
Kwa mujibu wa CAG, kwa miaka minne mfululizo ya 2020/2021 hadi 2023/2024, kiwango cha upatikanaji wa maji kwa mamlaka katika maeneo wanayotoa huduma kilikuwa kati ya asilimia 8 hadi 24.
Takwimu zinaonesha mwenendo wa kushuka kwa upatikanaji wa maji kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2021/2022, kutoka asilimia 24 hadi 11.
“Hali hiyo ilitokea kabla ya kutolewa kwa mwongozo wa mwaka 2022, na baadaye kuongezeka kidogo kutoka mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2023/2024, kutoka asilimia 8 hadi 9,” ripoti hiyo imeeleza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Maji iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji (Ewura) Machi 19, mkoani Morogoro, Waziri wa Maji, Juma Aweso, amesema Serikali itashirikiana na sekta binafsi kutoa huduma ya maji.
Aweso amesema watendaji wa Wizara ya Maji wanapaswa kuondokana na ubinafsi na kukubali mabadiliko, akibainisha kuwa Serikali inaandaa mazingira rafiki ya sekta binafsi kushiriki kikamilifu.
“Tumefanya mabadiliko ya sera, na sasa tunaelekea kwenye sheria ili kuruhusu sekta binafsi kufanya kazi ndani ya sekta ya maji,” amesema.
Katika maadhimisho ya Siku ya Maji 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua Sera ya Taifa ya Maji Toleo la 2025, amesema sera ya maji iliyoboreshwa inaongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kufadhili miradi ya maji na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya maji ili kuimarisha upatikanaji wa maji.
Kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Serikali imeahidi taifa ambalo kila mtu anapata huduma nafuu za maji safi na salama, sambamba na huduma bora za usafi ili kuimarisha afya ya jamii.
Kulingana na Wizara ya Maji, Tanzania inakadiriwa kuwa na rasilimali za maji zinazofaa kwa matumizi mbalimbali za wastani wa mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka.
Kiasi hicho kinahusisha maji juu ya ardhi, mita za ujazo bilioni 105, na maji chini ya ardhi, mita za ujazo bilioni 21 kwa mwaka.
Kwa idadi ya watu milioni 59.8 wa Tanzania Bara, kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kiasi cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,105.
Kiwango hicho kipo juu ya kiwango cha chini cha mita za ujazo 1,700 cha mahitaji ya maji kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa.
