Mpaja bado anapambana kufunga Uganda

MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Husna Mpaja, anayekipiga She Corporate FC ya Uganda amesema hajafunga bao hadi sasa akiamini bado ana muda wa kutia mpira wavuni.

Mpaja aliyejiunga na She Cooperate akitokea Rayon Sports ya Rwanda katika dirisha la usajili kwenye mzunguko wa pili, aliliambia Mwanaspoti anaamini muda wake bado kutokana na hatua anazopitia za kuzoea mfumo mpya wa timu.

“Nilipata muda mfupi sana kuwa na timu, kuanzia mashindano ya CECAFA hadi ligi kuu, hivyo sikuweza kupata muda wa kutosha wa kujiandaa na wenzangu,” alisema Mpaja na kuongeza licha ya changamoto hiyo, tayari ameanza kupata nafasi ya kucheza na kutoa asisti moja, akiendelea kupambana kuhakikisha anafunga mabao.

“Naanza kupata nafasi taratibu, nina asisti moja tayari na bado napambana kufunga. Nina imani muda wangu unakuja,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Mpaja, hadi sasa amecheza jumla ya mechi tatu na mbili aliingia akitokea benchi na moja alitokea benchi.

“Nimecheza mechi tatu, mbili nimetokea benchi na moja sikupata nafasi. Bado naangaliwa na makocha na kuingizwa taratibu kwenye mfumo wa timu pamoja na kuzoeana na wachezaji wenzangu.”