Mtanzania atambuliwa orodha viongozi bora wa masoko Afrika

Dar es Salaam. Mkuu wa Idara ya Masoko wa Benki ya Stanbic Tanzania, Neemarose Singo, ametajwa miongoni mwa viongozi 100 bora wa masoko barani Afrika, hatua inayoakisi kuimarika kwa mchango wa Watanzania katika uongozi wa chapa na mikakati ya biashara kwenye jukwaa la kimataifa.

Singo ameorodheshwa katika orodha ya Africa CMO 100 iliyochapishwa na taasisi ya Brand Africa, inayotambua viongozi waandamizi wa masoko kutoka Afrika na diaspora wenye ushawishi mkubwa katika kukuza taasisi, masoko na kujenga uaminifu wa wateja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Benki ya Stanbic Tanzania, orodha hiyo hujumuisha viongozi ambao mchango wao unaenda zaidi ya mawasiliano ya kawaida ya kibiashara, kwa kuweka mikakati inayochochea ukuaji wa taasisi na kuimarisha nafasi ya chapa katika ushindani wa soko.

Utambuzi huo unakuja wakati ambao Benki ya Stanbic Tanzania ikiendelea kuonesha mwelekeo chanya wa ukuaji na uimara wa kifedha. Ikiwa na zaidi ya miaka 30 ya uwepo nchini, benki hiyo imejijengea nafasi imara katika huduma za benki za makampuni, uwekezaji na biashara, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta muhimu kama miundombinu, biashara na ukuaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs).

Mwelekeo huo umeifanya Stanbic kuwa mdau muhimu katika mabadiliko ya sekta ya fedha na uchumi wa Tanzania, hasa katika kuimarisha ujumuishi wa kifedha na uwekezaji endelevu. Mwaka 2025, benki hiyo ilitunukiwa tuzo ya Benki Bora Tanzania na jarida la kimataifa la The Banker, ikitambua uimara wake wa kifedha, ubunifu wa huduma na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Katika mwendelezo wa mafanikio yake, mwaka 2026 benki hiyo imeshinda tuzo kadhaa za kimataifa kupitia Euromoney Private Banking Awards, zikiwemo Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalumu, Benki Bora kwa Kizazi Kijacho na Benki Bora kwa Huduma kwa Wateja. Tuzo hizo zinadhihirisha nafasi ya benki katika kusaidia wateja kujenga, kukuza na kulinda utajiri wao kwa mtazamo wa muda mrefu.

Akizungumza kutokana na utambuzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, amesema hatua hiyo inaakisi ubora wa uongozi ndani ya benki hiyo na nguvu ya taasisi kwa ujumla.

“Nafasi hii inaonesha kiwango cha juu cha uongozi ndani ya benki na thamani ya kimkakati ya chapa yetu. Chapa imara ni rasilimali muhimu inayojenga imani, kuongeza umuhimu na kusaidia azma yetu ya kuwahudumia wateja kwa ufanisi kadri sekta ya fedha nchini Tanzania inavyoendelea kukua,” amesema.

Rwegasira ameongeza kuwa, “Uongozi wa chapa barani Afrika unaendelea kubadilika. Sasa unahusu zaidi kujenga imani, kuelewa wateja na kutoa matokeo halisi ya biashara. Katika sekta ya benki, hili linamaanisha kuwawezesha wateja kushiriki kikamilifu katika mifumo ya kifedha.”

Orodha ya Africa CMO 100 inaonesha kuongezeka kwa umuhimu wa sekta ya huduma za kifedha katika kujenga uchumi jumuishi, huku viongozi wa masoko wakichukua nafasi muhimu katika kuunda taswira na mwelekeo wa taasisi hizi barani Afrika.

“CMO na viongozi waandamizi wa chapa ni miongoni mwa wabunifu wakubwa wa mustakabali wa Afrika. Kupitia mikakati, uongozi na ushawishi, wanaunda simulizi, wanajenga imani na kuongoza mwelekeo wa maamuzi ya mamia ya mamilioni ya watu,” amesema Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Brand Africa, Thebe Ikalafeng.

Ikalafeng ameongeza kuwa ACMO 100 ipo kutambua, kusherehekea na kuwaunganisha viongozi hao, na washindi wa kwanza wa Africa CMO 100 wanatarajiwa kutambuliwa rasmi katika Wiki ya Brand Africa itakayofanyika Addis Ababa, kuanzia Aprili 22 hadi Mei 26, 2026.