Misheni ya Artemis II ya Shirika la anga la Marekani NASA imekamilika rasmi Aprili 11, 2026 baada ya wanaanga wanne kurejea salama duniani kupitia “splashdown” katika pwani ya San Diego Ijumaa usiku (Huku kwetu ukiwa usiku wa kuamkia Jumamosi, wakikamilisha safari ya kihistoria ya siku 10 kuelekea Mwezi na kurudi.
Wanaanga hao, Victor Glover, Christina Koch, Jeremy Hansen na Kamanda Reid Wiseman, walirejea wakiwa katika hali nzuri kabisa, huku wakithibitishwa kuwa “green” na madaktari wa NASA.

Safari ya Kihistoria ya Siku 10
Safari ilianza Aprili 1, 2026, pale roketi ya Space Launch System ilipoondoka Kennedy Space Center, Florida. Wanaanga hao walitumia chombo cha Orion kilichopewa jina “Integrity”, wakisafiri mbali zaidi kuliko binadamu wengine wote waliowahi kufika tangu enzi za Apollo.
Kwa mujibu wa NASA, chombo hicho kilifika umbali wa takribani kilomita 406,771 kutoka Dunia, kikivunja rekodi ya zamani ya Apollo 13.
Changamoto za Kurudi Duniani
Wakati wa kurejea, chombo cha Orion kilikumbana na joto kali la hadi nyuzi 3,000°F wakati wa kuingia kwenye angahewa ya Dunia, ambapo pia kulitokea kukatika kwa mawasiliano kwa muda mfupi kutokana na mlipuko wa plasma.
Baadaye, mfumo wa parachute 11 ulisaidia kupunguza kasi ya chombo kabla ya kutua salama katika Bahari ya Pasifiki.

Uokoaji na Mapokezi
Baada ya kutua, wanaanga walitolewa kwenye chombo na kupelekwa kwenye meli ya uokoaji USS John P. Murtha, kabla ya kuhamishiwa hospitali ya uchunguzi wa awali na hatimaye kupelekwa Johnson Space Center.
Mafanikio na Maana ya Misheni
Misheni ya Artemis II imeweka rekodi mpya ikiwa ni safari ya kwanza ya binadamu kwenda mbali zaidi na Dunia tangu mwaka 1972, na pia imeleta mafanikio kadhaa ya kisayansi na kitabibu, ikiwa ni pamoja na utafiti wa mionzi, usingizi na mabadiliko ya mwili wa binadamu angani.
NASA imesema mafanikio haya yanafungua ukurasa mpya wa maandalizi ya kurejea kwa binadamu Mwezini na safari za baadaye kuelekea sayari ya Mars

