Canada. Leo tunaongelea kisa kingine cha Mswahili aliyeoa mama wa kizungu na kupata watoto na baadaye yakawakuta yaliyowakuta.
Bibby (si jina lake halisi) alikuwa mama aliyejaaliwa urembo si haba. Wengi walikuja kumchumbia akawakataa.
Alitaka aolewe na mume mwenye kujiweza na siyo wabangaizaji. Wanaume wengi kijini kwao walimuogopa kwa vile walijua alichokuwa akitafuta. Alizoea kueleza wazi wazi kuwa hawezi kutoa uzuri wake kwa mume asiye na uwezo.
Kijijini kwa Bibby kulikuwa na James mtoto wa maskini aliyebahatika kwenda majuu na kuukata.
Akiwa amewahi kutaka kumposa Bibby akamkataa, baada ya kuukata majuu alirejea nyumbani. Aliwajengea wazazi wake bonge la jumba na kuwanunulia gari.
Kila mmoja kijijini alitamani mwanawe angekuwa kama James. Mmoja wa waliotamani mafanikio ya James ni Bibby. Licha ya yote aliyofanya kijijini mwake, James alikamia kuwa angemuoa Bibby aliyekuwa kamkataa miaka ya nyuma.
Muda haukupita, Bibby alikwenda kwa wazazi wa James na kuomba namba yake ya simu. Wazazi walifurahi na kumpa namba ya simu. Bila ajizi, Bibby alimpigia simu James akiuliza ni kwanini alimsahau.
Kwa vile James alikuwa amekamia kumuoa, aliona kama ndege kajiingiza mtegoni mwenyewe. Hivyo, aliomba wakutane sehemu ya faragha lau waongee mawili matatu. Bibby alifurahi na kukubali kwenda kukutana na James. Wahenga waliasa. Usitukane mkunga na uzazi ungalipo na isitoshe hakuna ajuaye ya kesho.
Siku ya siku ilipofika, wawili walikutana kwenye hoteli moja maarufu mbali na kijijini kwao. Mambo yalikwenda haraka. Waliongea, wakala, wakanywa, wakapanga, hadi wakalala kule.
Haraka haraka, Bibby alimwambia James kuwa alikuwa akimpenda na wala hakumkataa bali kumpima uvumilivu wake ambao siku hii ulikuwa umelipa.
Mipango ya ndoa ilipangwa na ndoa ikafanyika tayari kuanza kuishi kama mke na mume. Moyoni mwa wawili hawa, kila mmoja alijifariji kuwa alikuwa amempata mwenzie wasijue wamepatikana wote. Kiukweli, Bibby hakumpenda James bali alitaka amtumia kama pasi ya kuingia majuu na mengine angejua huko huko.
Naye James hakumpenda Bibby bali alimtaka kutokana na urembo wake. Na alijua fika kuwa Bibby alikubali amuoe kwa vile alikuwa keshaukata na anaishi majuu. Nani angekataa fursa hii tena iliyojileta yenyewe kutoka kwa mtu ambaye amewahi kumuudhi kwa kumkatalia ndoa?
Wawili hawa walifunga ndoa. Muda wa James kuondoka kurudi majuu ulifika. Aliondoka na kumuacha Bibby kwa wazazi wake akimuahidi kumtumia tiketi au kumjia ili waende kuishi wote majuu.
Bibby na wazazi hata marafiki walifurahi sana. Muda haukupita, James akarudi kuja kuchukua mkewe ambaye alimuacha tayari mjamzito baada ya Bibby kumtegeshea mimba ili asibadili mawazo au kushawishiwa na mabinti wengine pale kijijini waliokuwa wakimmezea James mate.
Wawili waliondoka kwenda zao majuu. Baada ya Bibby kufika majuu mambo yalibadilika. James alianza kumnyanyasa na kumsimanga kuwa hakumpenda kwa dhati isipokuwa kwa sababu ya mafanikio yake jambo ambalo lilikuwa kweli.
Naye Bibby alijibu mapigo kwa kumwambia James kuwa hakumpenda bali kumtaka kwa uzuri wake na kumkomoa kiasi cha kumsimanga kwa mambo ya zamani.
Bibby alikuwa akiishi majuu kwa kutegemea vibali vya kuishi vya mumewe. Hivyo, asingeweza kufurukuta bali kuvumilia hadi apate vyake. Muda ulizidi kwenda na Bibby akaongeza watoto wawili huku akipanga kulipiza kisasi siku ambayo angepata vibali vyake amuache James na kuanza maisha yake akiwa mtu huru.
Muda haukupita Bibby akapata vibali. Bila kungoja, alimwambia mumewe nia yake ya kutaka kuachana. Kabla ya kufanya hivyo, Bibby alipata ushauri kuwa kwa vile watoto wao walikuwa bado wachanga, kama wangeachana, angebaki na watoto na serikali ingemsaidia kuwatunza na pia kwa kumlazimisha James atoe pesa ya matunzo ya familia.
Kwa kuwa na haki ya kukaa na watoto, pia Bibby alipata haki ya kubaki na nyumba yao. Hili, halikuingia akilini mwa James aliyembembeleza warudi nyumbani Afrika walimalize. Bibby alikataa katakata.
James aliamua kumuua kwa kumpiga na kitu kizito na kunyonga watoto wao na kukimbia hadi alipokamatwa na kufungwa maisha na ndoa ya majuu ikaishia kuwa maanguko ya wote.
