Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (NJE Sports) imepoteza kwa mabao 3–2 dhidi ya timu ya Ubalozi wa Umoja wa Ulaya katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Aprili 11, 2026, kwenye Uwanja wa John Merlin, jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa James Milya (Mb), amezipongeza timu zote mbili kwa kuonesha ushindani wa kirafiki na kudumisha mshikamano. Amesema michezo ya aina hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano, urafiki na diplomasia kati ya taasisi na mataifa.
Ameongeza kuwa mechi hiyo ni sehemu ya juhudi za kukuza diplomasia ya michezo, sambamba na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Wizara na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya.
Mchezo huo pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, ambaye amesema kuwa pamoja na ushindani uliokuwepo uwanjani, lengo kuu la mchezo huo lilikuwa kuimarisha uhusiano kati ya pande husika, akisisitiza kuwa huo ndio ushindi mkubwa zaidi kuliko mabao.
Kwa upande wake, kiongozi wa timu ya Ubalozi wa Umoja wa Ulaya, Bw. Ally Mwinchade, amesema ameridhishwa na kiwango cha ushindani kilichooneshwa na timu zote mbili, akieleza kuwa mchezo huo umeimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki kati ya pande hizo.
Ameongeza kuwa ushindi huo si matokeo ya uwanjani pekee, bali pia ni ishara ya mshikamano, ushirikiano na dhamira ya kuendeleza diplomasia kupitia michezo. Aidha, ameipongeza timu ya NJE Sports kwa kuonesha mchezo mzuri na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika michezo ijayo.
.jpeg)





.jpeg)





.jpeg)
