Ripoti ya CAG yaanika madudu Pamba, Dodoma Jiji

RIPOTI ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya ukaguzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2024/25 imezigusa timu mbili za Ligi Kuu Bara pamoja na moja ya Ligi ya Championship.

Timu za Ligi Kuu ambazo zimeanikwa na Ripoti ya CAG ni Pamba Jiji ya Mwanza na Dodoma Jiji ya Dodoma huku ya Championship ikiwa ni Geita Gold.

Ripoti hiyo imebainisha matumizi yaliyozidi na yasiyotengewa bajeti ya kiasi cha Sh2.13 bilioni kwa ajili ya klabu hizo zinazomilikiwa na halmashauri za majiji ya Dodoma na Mwanza pamoja na ya mji wa Geita.

Dodoma Jiji licha ya kupanga kutumia bajeti ya Sh745 milioni, ripoti hiyo imebaini ilitumia Sh1.17 bilioni wakati Geita Gold yenyewe ikipoea kiasi cha Sh718.48 milioni kiasi cha tofauti na kile ambacho ilikipanga cha Sh500 milioni. “Hata hivyo, Halmashauri zinazomiliki klabu za michezo ikiwepo Halmashauri ya Geita na Halmashauri ya Jiji la Mwanza zilitumia jumla ya Sh2.13 bilioni kwenye klabu hizo. Pamba Jiji FC ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilitumia Sh1.48 bilioni, matumizi ambayo hayakuwa kwenye bajeti ya mwaka iliyoidhinishwa,” imebainisha.

Ripoti hiyo imefafanua kwamba, Geita Gold ya Halmashauri ya Geita, ilitengewa Sh500 milioni lakini ilipokea Sh718.48 milioni na kusababisha matumizi ya ziada ya Sh218.48 milioni. Vilevile, Halmashauri ya Jiji Dodoma ilipanga bajeti ya Sh745 milioni kwa Dodoma Jiji FC lakini ilitoa Sh1.17 bilioni, hivyo kuzidisha kiasi cha Sh427.70 bilioni.

Ripoti hiyo imesema kwamba hakukuwa na bajeti ya ziada, mapitio mapya ya bajeti au kibali rasmi kilichotolewa ili kuhalalisha matumizi hayo ya ziada, jambo linaloashiria upangaji na udhibiti usioridhisha wa bajeti.

Kupitia ripoti hiyo, TAMISEMI imepewa pendekezo la kuhakikisha inaimarisha usimamizi kwa menejimenti za Halmashauri ili kuhakikisha kuwa hakuna matumizi yanayofanyika bila idhini au bajeti ya nyongeza iliyoidhinishwa kisheria, na kwamba bajeti halisi ziendane na mipango madhubuti na endelevu iliyoandaliwa kabla ya fedha kutolewa. Juhudi za kuwatafuta Wakurugenzi wa Halmashauri zinazomiliki timu hizo ili watoe ufafanuzi juu ya ripoti hiyo ziligonga mwamba kwani simu zao ziliita bila kupokelewa.