Dar es Salaam. Wizara ya Uchukuzi imeahidi kuchukua hatua za haraka, kutatua changamoto tano zinazokwamisha sekta ya usafirishaji wa barabarani, ikiwemo utozwaji wa tozo kwa madereva wa Tanzania wanapotumia barabara nchini Zambia.
Changamoto nyingine ni mamlaka za serikali ikiwemo halmashauri na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kuja na ada mpya kila wakati.
Changamoto hizo zimeelezwa na Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Wasafirishaji Mizigo kwa Barabara Tanzania (TRFA), Hussein Wandwi Aprili 11, 2026 katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam, Mgeni Rasmi akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Profesa Godius Khayarara.
Mtendaji Mkuu wa TRFA, Hussein Wandwi akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa chama hicho
“Miongoni mwa changamoto zinazotusibu ni tozo mpya za barabara za Zambia pia zinaongeza gharama za kufanya biashara, kama watatoza malori yetu, tunapaswa pia kuwatoza malori yao,”amesema na kuongeza;
“Pia wasafirishaji wanatakiwa na halmashauri kulipa tozo ya huduma ambayo zamani ilikuwa ni asilimia 0.3 na sasa 0.25 ya turnover kila robo ya mwaka, hii ni kodi ambayo tunaomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha iiangalie kwani wasafirishaji wanalipa kodi nyingi,” amependekeza.
Mbali na hayo, Wandwi ameiomba Serikali, iwarasimishe mawakala wa usafirishaji wasio na ofisi ili wawepo kwenye vyama vya wasafirishaji kama mawakala wanaojulikana wenye vitambulisho na wasajiliwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia Wandwi amesema wasafirishaji hawatendewi haki na wenye mzigo au wakala kuhusu malipo hivyo akitaka Serikali kutafuta suluhisho la tatizo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi Msaidizi Usafiri kwa njia ya Barabara Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana amesema wizara hiyo inatambua mchango wa TRFA katika kutetea masilahi ya wanachama na kuboresha ushirikiano baina ya wanachama na serikali.
“TRFA mmekuwa mkiwasilisha changamoto ya Zambia kuhusu tozo ya matumizi ya barabara, Serikali inaruhusu watu kuwekeza wenzetu wana wawekezaji wa barabara. Mmepata hizo tozo tumeshawasiliana na Serikali ya Zambia kuwaomba hilo swala liangaliwe,” amesema.
Akizungumzia foleni ya malori Tunduma, Magombana amesema Serikali ya Tanzania na Zambia zinashughulika kwa pamoja na matarajio baada ya muda mpaka huo utakuwa sehemu ya kupita na sio sehemu ya kusimama.
Magombana amesema sekta ya uchukuzi itaendelea kuwa imara na kuboresha mazingira ya wezeshi katika kukuza uchumi wa nchi.
“Napenda kuhakikishia kuwa Wizara ya Uchukuzi itaendelea kuzitatua changamoto zilizo chini yake na kuziwasilisha changamoto zilizopo nje yake kwa taasisi husika ili ziweze kufanyiwa kazi kikamilifu,” amesema.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa njia ya Barabara Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana (mwenye kaunda suti nyeusi)akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) pamoja na wa Chama Cha Wasafirishaji wa Mizigo kwa Barabara Tanzania ( TRFA) kwenye mkutano wa mwaka wa TRFA
Akizungumzia utendaji wa bandari, Magombana amesema bandari Tanga, Dar es Salaam na Mtwara zimehudumia shehena za tani milioni 19.9 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, hatua inayoashiria ukuaji wa sekta ya uchukuzi na biashara ya kimataifa.
Amefafanua kuwa kiwango hicho kitakuwa ongezeko ikilinganishwa na tani milioni 32.75 zilizohudumiwa katika mwaka uliopita wa fedha 2024/2025.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa ongezeko hilo la mizigo, hasa inayosafirishwa kwenda nchi jirani, linahitaji maboresho ya haraka katika mifumo ya usafirishaji wa ndani ili kuhakikisha ufanisi unakuwepo kuanzia bandarini hadi kwa mlaji wa mwisho.
“Ndugu washiriki, ongezeko la mzigo katika bandari zetu, hususan inayokwenda nchi jirani, linahitaji ufanisi mkubwa katika usafirishaji kutoka bandarini hadi maeneo ya mwisho kwa wateja husika,” ameongeza.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TRFA, Sophia Mansoor amesema chama hicho kitaendeleza ushirikiano na Serikali katika kutatua sekta ya usafirishaji katika kuchochea maendeleo na uwekezaji katika sekta hiyo.
Sophia amesema Tanzania inahudumia nchi nyingi kutokana na kuwepo bandari, hivyo lazima kuangalia sekta ya usafirishaji kwa jicho la pekee ili kufanya uwekezaji uendelee kuwepo.
