Dar es Salaam. Viongozi wa Serikali, wataalamu wa afya na madereva wa pikipiki maarufu bodaboda, leo Aprili 12, 2026, wameungana katika matembezi ya mshikamano yaliyolenga kutoa elimu na kuhamasisha matumizi sahihi ya kofia ngumu (helmet) ili kupunguza madhara ya ajali barabarani.
Tukio hilo ni maandalizi kuelekea mkutano wa pili wa kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, unaotarajiwa kuwakutanisha wataalamu mbalimbali wa afya kujadili mbinu za kisasa za matibabu na kinga dhidi ya magonjwa na majeraha ya mfumo wa fahamu, Aprili 16, 2026, katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Matembezi hayo yameanza katika eneo la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), yakihusisha pia mazoezi ya viungo kama sehemu ya kuhamasisha afya bora kwa jamii.
Akiongoza tukio hilo, Mganga Mkuu wa Serikali, Grace Magembe, amesisitiza umuhimu wa madereva wa bodaboda kuvaa helmet muda wote wanapokuwa barabarani, akieleza kuwa majeraha ya kichwa ni miongoni mwa sababu kuu za vifo na ulemavu vinavyotokana na ajali.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dk Rahma Hingora akiwa katika mazoezi ya viungo
Amesema, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wa afya, bado kumekuwepo na mwitikio mdogo wa matumizi ya helmet kwa baadhi ya madereva, jambo linaloongeza hatari ya madhara makubwa wanapopata ajali.
“Ni muhimu kwa kila dereva wa bodaboda kuelewa kuwa helmet si chaguo, bali ni ulinzi wa maisha yake. Ajali inaweza kutokea wakati wowote, hivyo tahadhari ni jukumu la kila mmoja,” amesema Dk Magembe.
Kwa upande wao, baadhi ya madereva wa bodaboda walioshiriki matembezi hayo wamesema elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa inawakumbusha wajibu wao wa kujilinda pamoja na abiria wao.
Wakati juhudi hizi zikiendelea, takwimu zinaonesha kuwa ajali za bodaboda bado ni tishio kubwa nchini. Kufikia Machi 2026, baadhi ya maeneo yaliendelea kushuhudia ongezeko la ajali, hali inayotia wasiwasi kwa wadau wa usalama barabarani na afya.
Kwa mujibu wa taarifa, mwezi Februari 2026, Wilaya ya Kati iliripoti ajali 36, ikiwa kinara kwa takribani asilimia 19.4 ya ajali zote zilizorekodiwa katika kipindi hicho. Wataalam wanaeleza kuwa hali hii inaonesha mwenendo unaohitaji hatua za haraka za udhibiti.
Aidha, Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI) imeendelea kupokea mzigo mkubwa wa majeruhi, ikihudumia wastani wa wagonjwa 700 kwa mwezi, ambapo takribani asilimia 60 wanatokana na ajali za bodaboda. Hii inaashiria ukubwa wa tatizo hilo katika sekta ya afya.
Utafiti unaonesha kuwa chanzo kikuu cha ajali hizo ni mwendo kasi (asilimia 63), uzembe wa madereva (asilimia 58), pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara (asilimia 51). Pia, ukosefu wa elimu ya usalama barabarani umetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha ukaguzi wa vyombo vya moto pamoja na matumizi ya teknolojia ya kamera za usalama, hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa kama Ubungo na Kimara.
Wataalamu wa afya waliopo kwenye matembezi hayo wameeleza kuwa kampeni kama hizi zina mchango mkubwa katika kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani, hasa kwa kundi la madereva wa bodaboda ambao wako hatarini zaidi.
