Sh230 bilioni za NMB zilivyochochea mageuzi, uwekezaji

Dar es Salaam. Benki ya NMB imeendelea kujipambanua kama kinara wa mageuzi ya sekta ya fedha nchini, ikiwekeza kwa kiwango kikubwa katika teknolojia na ubunifu ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita hadi kufikia mwaka jana.

Uwekezaji huo si tu kwamba umechochea upatikanaji wa huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, bali pia umeboresha huduma hizo na kuimarisha ushindani wa sekta hiyo katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP 2020/21–2029/30).

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Benki Bima, Martine Massawe, kati ya mwaka 2021 na 2025, benki hiyo iliwekeza zaidi ya Sh230 bilioni katika teknolojia za kisasa, ikilenga kuimarisha mifumo ya ndani, kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja, na kufungua fursa mpya za kifedha kwa makundi mbalimbali ya wananchi, huku ikichangia pia ujumuishaji wa kifedha.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Sekta ya Fedha 2026 jijini Dar es Salaam, Massawe amesema mkakati wa benki hiyo ni kutumia teknolojia na ubunifu ili kutoa suluhisho jumuishi na endelevu.

Mkutano huo, ulioratibiwa na Wizara ya Fedha, uliwakutanisha watunga sera na viongozi wa sekta ili kutathmini utekelezaji wa FSDMP na kuoanisha vipaumbele na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema uwekezaji wa kila mwaka katika teknolojia umeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka Sh18 bilioni mwaka 2021 hadi Sh43 bilioni mwaka jana, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikielekezwa katika kuimarisha mifumo ya msingi ya kibenki na miundombinu ya kidijitali.

Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji huo umeongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma, ambapo idadi ya wateja wa NMB iliongezeka kutoka milioni 4.6 hadi milioni 9.9.

Mtandao wa uwakala pia umepanuka kutoka mawakala 8,400 hadi zaidi ya 73,000, huku idadi ya matawi ikiongezeka kutoka 226 hadi 246.

“Takwimu hizi si ukuaji wa kawaida tu, zinaashiria ongezeko la upatikanaji wa huduma kwa wananchi,” amesema wakati wa mjadala kuhusu ubunifu, teknolojia na Akili Unde (AI) katika sekta ya fedha, na kuongeza kuwa uwekezaji katika teknolojia pia umechangia kupanua matumizi ya huduma za bima.

Kupitia mifumo ya kidijitali kama NMB Mkononi na NMB Jirani, benki imefanikiwa kubadilisha utoaji wa huduma za bima kwa kuzifanya ziwe rahisi na nafuu.

Bidhaa kama Mkono wa Pole wa Faraja zinaendelea kuwavutia maelfu ya wateja wapya kila mwezi kwa gharama nafuu inayoanzia TZS 200 tu.

Akijibu hoja kuhusu athari za teknolojia kwa ajira, Massawe amebainisha kuwa teknolojia haikusudii kuchukua nafasi ya binadamu, bali kuongeza uwezo wao wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Teknolojia inapanua uwezo wa binadamu, inaongeza ufanisi, inafungua fursa mpya, na inawawezesha wafanyakazi kutoa thamani zaidi kupitia ubunifu,” amesema.

Mageuzi yanayofanywa na NMB yanaendana na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambazo zinalenga kujenga mfumo wa kifedha jumuishi, thabiti na unaotumia teknolojia mpya na za kisasa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko ya Fedha wa NMB, Gladness Deogratias, amesema hati fungani ya Jasiri ni mfano halisi wa jinsi sera zinavyoweza kutafsiriwa na kutekelezwa kwa vitendo.

Ameeleza kuwa benki ilitumia fursa zilizotolewa na sera mpya za kifedha kubuni bidhaa inayowalenga wanawake na vijana wajasiriamali, ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto ya ukosefu wa dhamana licha ya kuwa na biashara zenye uwezo wa kukua.

“Kwa mantiki hiyo, mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha haukutupatia tu ujasiri, bali pia ulitupatia uhalali na mfumo madhubuti wa kuendeleza ubunifu ndani ya taasisi na katika soko kwa ujumla,” amesema.