Dar es Salaam. Wakati Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unaonesha kuwa Serikali ilitumia Sh84.74 trilioni kulipa fidia kati ya mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025, sekta zilizoongoza kwa kupata ajali kazini ni viwanda, ujenzi, umeme na gesi, pamoja na usafirishaji.
Fidia hizo zilihusisha ulemavu wa muda au wa kudumu, huduma za uangalizi, gharama za mazishi, na misaada ya matibabu, kwa mujibu wa sheria.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebainisha hayo katika ripoti yake iliyokabidhiwa bungeni Aprili 10, 2026, ikiwa ni matokeo ya alichokibaini kwenye usimamizi wa ukaguzi wa usalama na afya kazini (OSHA) katika maeneo ya kazi.
Aidha, matokeo yanahusu pia ufanisi wa hatua za uangalizi zinazochukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ili kuhakikisha kuwa ukaguzi wa OSHA katika maeneo ya kazi unafikia malengo yaliyokusudiwa ya usalama na afya kazini.
Katika ukaguzi, ripoti hiyo imeeleza kubaini kiasi hicho cha fedha kimetumika katika kulipa fidia, huku ajali nyingi zikitokana na kiwango kidogo cha uzingatiaji wa kanuni za usalama.
Kuhusu kiwango cha upungufu wa ajali na magonjwa ya kazini katika maeneo ya kazi, ripoti hiyo imesema upungufu wa ajali na magonjwa ya kazini huathiriwa na uwepo wa kanuni madhubuti na utekelezaji wake unaoimarisha uzingatiaji wa viwango vilivyowekwa.
“Mapitio ya Ripoti za Utekelezaji wa Mwaka kuanzia 2020/2021 hadi 2024/2025 yanaonesha kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha uzingatiaji wa masuala ya OSHA katika maeneo ya kazi.
“Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa utekelezaji wa OSHA, kuandaa miongozo ya mifumo yake ya usimamizi, pamoja na kusajili na kukagua maeneo ya kazi,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo, uchambuzi wa ripoti hizo umebaini kuwa kiwango cha ajali kazini kilipungua kutoka ajali 3,155 mwaka 2020/2021 hadi ajali 1,355 mwaka 2024/2025.
Kwenye ajali, ukaguzi huo umebaini OSHA haikufanikiwa kufikia lengo lake chini ya lengo D la mpango mkakati wa mwaka 2021–2026, ambalo lililenga kupunguza ajali na magonjwa ya kazini.
“Moja ya malengo ilikuwa kupunguza ajali kwa kuhamasisha maeneo ya kazi kutekeleza mkakati wa ‘Vision Zero’ na kufanya ufuatiliaji wa kila mwaka ifikapo 2026.
“Hata hivyo, hatua hii haikuingizwa kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli zake, hivyo kushindwa kufikia malengo ya kupunguza ajali zilizoripotiwa,” imesema.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya ajali ilipungua kwa asilimia 57 kutoka 3,155 mwaka 2021/2022 hadi 1,355 mwaka 2024/2025, lakini bado haikufikia lengo la kupunguza hadi ajali 1,000 kwa mwaka.
Pia, wakala huo ulishindwa kufikia malengo ya kupunguza magonjwa ya kazini. Ingawa kulikuwa na upungufu wa visa vya magonjwa ya kazini, idadi hiyo iliendelea kuwa juu ya malengo yaliyowekwa, ambapo lengo lilikuwa kushuka hadi visa 23 ifikapo 2024/2025.
Kwa upande wa vifo, ripoti imebainisha kuongezeka kwa vifo kazini kwa asilimia 22 kutoka 76 mwaka 2020/2021 hadi 161 mwaka 2022/2023, kisha kushuka na kupanda tena hadi 93 mwaka 2024/2025, hali inayoonesha kutokuwepo kwa mwelekeo thabiti wa upungufu.
Pamoja na hayo, ripoti imeeleza kwamba kumekuwepo na ukosefu wa takwimu jumuishi za ajali, ambapo ukaguzi ulibaini kuwa Serikali haikuwa na takwimu kamili kutoka OSHA na WCF.
“Taarifa za taasisi hizi zilikuwa zinatofautiana, ambapo OSHA ilionesha kupungua kwa ajali huku WCF ikionesha kuongezeka. Hii inaashiria udhaifu katika uratibu na ufuatiliaji.
“Aidha, hakukuwa na mfumo wa pamoja wa takwimu, pamoja na ukosefu wa taarifa za tathmini ya utekelezaji wa sera ya OSHA,” imesema ripoti hiyo.
Vilevile, imebainika kuwepo kwa usajili hafifu wa maeneo ya kazi, ambapo OSHA imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha mfumo wa usajili wa mtandaoni (WIMS) na kuondoa ada za usajili ili kuhamasisha usajili, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
Changamoto hizo ni pamoja na asilimia 79 ya maeneo ya kazi hayajasajiliwa. Kati ya maeneo 179,196 yaliyobainishwa, OSHA ilisajili 37,382 pekee, sawa na asilimia 21, huku asilimia 79 ikiwa haijasajiliwa.
Hata hivyo, ripoti imesema OSHA ilivuka malengo ya usajili. Licha ya changamoto hizo, maeneo 48,906, sawa na asilimia 140 ya lengo lake la kusajili maeneo 35,000 ifikapo 2026, yalisajiliwa.
Kuhusu ukosefu wa utekelezaji wa adhabu, ripoti imeeleza kuwa licha ya maeneo 11,578 kuwa yakifanya kazi bila usajili, hatua za kisheria hazikuchukuliwa ipasavyo, kinyume na sheria inayotaka kutozwa faini kati ya Shilingi milioni moja hadi tano.
“Kwa ujumla, ukosefu wa usajili wa kutosha unadhoofisha uwezo wa OSHA kufuatilia na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi, kwani maeneo mengi hubaki nje ya ukaguzi rasmi,” imesema ripoti hiyo.
Katika mapendekezo, ripoti hiyo, pamoja na mambo mengine, imetaka OSHA kuimarisha ushirikiano na taasisi za udhibiti ili kusaidia kubaini maeneo ya kazi ambayo hayajasajiliwa na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sheria za usalama na afya kazini.
Kwa upande wa Wizara ya Kazi, ripoti hiyo imeitaka kubadilishana maarifa kwa utaratibu maalumu, pamoja na kujenga uwezo ili kuimarisha utekelezaji wa sheria na kuhimiza ufuataji wa viwango vya usalama na afya kazini.
Pia, kuanzisha mfumo wa kati wa usimamizi wa taarifa za usalama na afya kazini utakaojumuisha takwimu kutoka OSHA na WCF, ili kuhakikisha uwiano na ulinganifu katika utoaji wa taarifa kuhusu ajali za kazini, vifo na gharama za fidia zinazohusika.
