Simba imetoka nyuma na kuichapa Dodoma Jiji kwa mabao 3-1, ikijihakikishia kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku Singida BS ikiitupa nje Mbeya City.
Simba ililazimika kusubiri mpaka kipindi cha pili kwa mashabiki wake kushangilia mabao hayo matatu yakifungwa na Seleman Mwalimu aliyetikisa nyavu mara mbili sambamba na Anicet Oura na kuirudisha klabu hiyo kwenye njia ya ushindi.
Wageni Dodoma ndio waliotangulia kubadilisha ubao wa matokeo, ikiwachukua dakika tisa tu kupata bao la kuongoza likifungwa na kiungo Khleffin Hamdoun ‘Fini’ kwa shuti la mguu wa kushoto akiunasa mpira uliokuwa ukigombewa na beki wa Simba Rushine De Reuck ambaye aliukosea ukatua miguuni kwa mfungaji.
Hilo lilikuwa shuti pekee kwa Dodoma lililolenga lango kwani baada ya bao hilo, Simba ndio ilitawala kipindi hicho cha kwanza ikitafuta bao la kusawazisha lakini ukuta wa wageni ulikuwa makini kuzima mashambulizi hayo.
Mpaka mapumziko Dodoma ilitoka na uongozi wa bao 1-0 lakini ikitumia muda mwingi kuzuia jambo ambalo lilikuwa hatari kwao, kwa kuwa Simba ilitengeneza nafasi nyingi za wazi kwenye mchezo huo.
Kipindi cha pili iliwachukua Simba dakika tisa kupata bao la kusawazisha likipatikana dakika ya 54 mfungaji akiwa Mwalimu ambaye alisawazisha makosa yake kufuatia kupoteza nafasi za wazi kipindi cha kwanza, akifunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Nickson Kibabage ambaye alionyesha uwezo wa juu kwenye mchezo huo.
Dodoma itajilaumu yenyewe ikishindwa kushikilia ‘bomba’ kufuatia kukaa nyuma kwa muda mrefu, ikicheza mchezo wa kujilinda na kuwaachia wenyeji kutengeneza mashambulizi mengi na kuzaa matunda dakika ya 54.
Wakati Dodoma inajiuliza ikaruhusu bao la pili dakika ya 60 likifungwa na winga Oura kwa shuti kali akimalizia pasi ya Clatous Chama.
Msumari wa tatu kwenye mchezo huo uliwekwa na Mwalimu tena dakika ya 67 akiwarudisha kati Dodoma akitangulia kuwachambua mabeki wa Dodoma na kumfunga kirahisi kipa Daniel Mgore ambaye alifanya kazi kubwa kwenye mchezo huo.
Mpaka mwisho wa mchezo wa mchezo Simba ilitoka kifua mbele kwa ushindi huo wa mabao 3-1,ikitinga hatua ya robo fainali kibabe ikiungana na Yanga.
Matokeo mengine yalishuhudia TRA United nayo ikisonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo, Singida Black Stars ikiiua Mbeya City kwa mabao 5-1.
Kabla ya mchezo wa jana kati ya Azam na Fountain Gate, timu za Yanga, TRA, Singida, Simba, Coastal, Mashujaa na JKT Tanzania zimeshafuzu hatua ya robo fainali.