Takukuru yatangaza ajira mpya 500, vigezo hivi hapa

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza nafasi 500 za ajira kwa Watanzania wenye sifa, hatua inayolenga kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika ngazi za wilaya kote nchini.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, nafasi zilizotangazwa zinahusisha ofisa uchunguzi 250 pamoja na wachunguzi wasaidizi 250, watakaofanya kazi katika ofisi za Takukuru wilayani.

Kwa upande wa nafasi za ofisa uchunguzi, waombaji wanatakiwa kuwa na angalau shahada ya kwanza katika fani mbalimbali, zikiwemo sheria, uhasibu, uchumi, uhandisi, Tehama na nyingine zinazotambulika na Serikali.

Aidha, waombaji wanapaswa kuwa na ufaulu usiopungua daraja la pili la chini, huku wale waliosajiliwa na bodi za kitaaluma wakipewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, waombaji wa nafasi hizo hawapaswi kuzidi umri wa miaka 29 ifikapo Mei, 2026.

Kwa upande wa nafasi za mchunguzi msaidizi, Takukuru imesema waombaji wanapaswa kuwa na cheti au stashahada katika fani mbalimbali, zikiwemo ulinzi, udereva, ufundi magari, uhasibu, ukatibu muhtasi na Tehama, kulingana na mahitaji ya kazi husika. Waombaji wa nafasi hizi wanatakiwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 25.

Mbali na sifa za kitaaluma, taasisi hiyo imesisitiza kuwa waombaji wote wanapaswa kuwa na uadilifu wa hali ya juu, kutokuwa na rekodi ya uhalifu, na kuwa tayari kufanya kazi katika wilaya yoyote Tanzania Bara.

Pia, waombaji wametakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu, zikiwemo vyeti vya masomo, cheti cha kuzaliwa, wasifu binafsi (CV), pamoja na majina ya wadhamini watatu wa kuaminika. Aidha, matumizi ya vyeti vya kughushi au taarifa za uongo yameonywa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Katika utaratibu wa uwasilishaji maombi, Takukuru imeelekeza kuwa maombi yote yatumiwe kupitia mfumo wa kielektroniki wa ajira wa taasisi hiyo, huku maombi ya posta au kwa mkono yakisisitizwa kutokubalika.

Barua za maombi zinapaswa kuelekezwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, makao makuu yaliyopo Dodoma.

Mwisho wa kutuma maombi umetajwa kuwa Mei 3, 2026, na waombaji watakaofanikiwa katika hatua ya awali ya mchujo ndio watakaowasiliana kwa hatua zinazofuata.

Tangazo hilo linatarajiwa kuvutia maelfu ya vijana nchini, hasa ikizingatiwa changamoto ya ajira na umuhimu wa taasisi hiyo katika kusimamia uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.