TRAMEPRO Yatoa Tahadhari Kuhusu Uharibifu wa Fukwe za Ziwa Victoria

Uharibifu wa Ziwa Victoria: Matokeo ya Shughuli za Kibinadamu Yaanza Kuonekana Wazi

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la shughuli za kibinadamu kandokando ya Ziwa Victoria, hali ambayo sasa imeanza kuleta athari zinazoonekana wazi katika mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), ukiongozwa na Katibu Mkuu wake, Boniventura Mwalongo, umebaini changamoto kadhaa zinazolikumba ziwa hilo. Ziara hiyo ilifanyika katika eneo la Kigoto, Mwanza, kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu (TAHURI).

Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni pamoja na uwepo wa magugu vamizi, matumizi holela ya rasilimali za ziwa, pamoja na uchafuzi wa maji unaotokana na majitaka yasiyodhibitiwa.

Aidha, kupungua kwa kina cha maji kumetajwa kuwa matokeo ya moja kwa moja ya uharibifu wa maeneo ya kinga ya fukwe, jambo linalochangia kuongezeka kwa tope na mchanga ndani ya ziwa. Hali hii inaathiri kwa kiasi kikubwa mazalia ya samaki na kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa rasilimali hiyo muhimu.

Wataalamu wanaonya kuwa endapo hali hii itaendelea, usalama wa chakula, ajira za wavuvi na uchumi wa maeneo yanayozunguka ziwa hilo vitakuwa hatarini.