TIMU ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars imeingia rasmi kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa FIFA Series dhidi ya Morocco.
Kikosi hicho tayari kimeondoka nchini kwenda Morocco kwenye maandalizi ya mwisho, huku benchi la ufundi likitumia mechi hiyo kama kipimo cha kiwango cha wachezaji dhidi ya timu kubwa Afrika.
Taarifa kutoka ndani ya timu zinaeleza kuna uwezekano mkubwa wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi kutokuwepo kwenye kikosi hicho kutokana na changamoto mbalimbali za upatikanaji wao dirisha hili.
Katika kikosi hicho, zaidi ya wachezaji 15 wametoka kwenye klabu ya JKT Queens jambo linaloifanya timu hiyo kuwa na uwakilishi mkubwa Twiga Stars.
“Wachezaji wengi wa kigeni watakosa mechi kutokana na majukumu mengi ya timu zao halafu wametoka muda si mrefu kwenye maandalizi ya WAFCON,” kilisema chanzo na kuongeza;
“Hivyo kwa kuwa ni mechi ya kuangalia uwezo wa wachezaji kwa wale watakaopatikana nje na hawa wa ndani watachanganyika ili tuone tunafanyaje.”
