Dar es Salaam. Uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke huwa na hatua mbalimbali, ikiwamo kipindi ambacho hisia za mapenzi hupungua au kuisha. Mara nyingi, dalili za mabadiliko haya hutofautiana kati ya mwanaume na mwanamke.
Kutozitambua dalili hizi kunaweza kumfanya mmoja kuendelea kung’ang’ania uhusiano akidhani bado upo imara, ilhali tayari umeanza kudhoofika. Kadiri mtu anavyochelewa kugundua hali hiyo, ndivyo maumivu yanavyoweza kuwa makubwa zaidi.
Mwanaume huanza kuonyesha hasira na kukasirika kwa urahisi hata kwa mambo madogo. Hali hii hutokana na kupungua kwa hisia za mapenzi, hivyo kukosa uvumilivu.
Anaweza kukujibu kwa ukali hata mbele ya watu bila kujali unavyojisikia. Tofauti na awali alipokuwa mvumilivu, mabadiliko haya ni ishara kuwa penzi limeanza kupoa au kuisha.
Kwa kawaida mwanaume anayependa hujitahidi kumfurahisha mwenza wake. Hufanya mambo mbalimbali ili kuhakikisha anapata furaha na kuridhika katika uhusiano.
Hata hivyo, mapenzi yanapopungua, juhudi hizi hutoweka. Hamu ya kuona mwenza wake akiwa na furaha hupungua au kuisha kabisa.
Kupungua kwa muda wa kuwa pamoja ni dalili nyingine. Mwanzoni mlikuwa na muda wa kutosha wa kuwa pamoja, lakini hali hubadilika ghafla.
Anakuwa na visingizio vingi kama kazi, safari, uchovu au majukumu, vinavyomfanya akose muda wa kuwa na wewe. Mara nyingi, huonekana kuwa na muda zaidi kwa marafiki kuliko kwa mwenza wake. Hii ni ishara muhimu ya tahadhari.
Mwanaume anapoacha kupenda hupunguza au kuacha kabisa kujali na kumhudumia mwenza wake.
Hali ya kukufanya ujisikie wa pekee hupotea. Wakati mwingine anaweza kuwa mwema na kuwajali wengine, lakini si wewe. Upendo na ukaribu uliokuwapo awali hupungua kwa kiasi kikubwa.
Mawasiliano huwa magumu. Mwanaume huanza kuwa mzito kuzungumza na kuonyesha hisia zake.
Tofauti na awali alipokuwa akikusikiliza na kushirikiana nawe, sasa anaonekana kutojali. Hata kuuliza alipo au anachofanya kunaweza kusababisha mvutano. Hii ni dalili kuwa uhusiano uko hatarini.
Mwanaume anayependa huwa wazi kuhusu maisha yake. Hushirikisha mwenza wake mambo mengi bila kuficha.
Lakini mapenzi yanapopungua, siri huongezeka. Unakosa ufahamu wa kinachoendelea katika maisha yake, na haoni umuhimu wa kukushirikisha mambo yanayomhusu.
Kupungua kwa ushirikiano wa kihisia ni dalili nyingine. Furaha au mafanikio yako hayampi tena msisimko kama ilivyokuwa awali.
Kila mmoja anaonekana kuishi maisha yake binafsi, hata kama mnaishi pamoja. Uhusiano hugeuka kuwa kama wa watu wanaoishi nyumba moja bila ukaribu wa kimapenzi.
Kwa ujumla, dalili hizi zinaonyesha mabadiliko katika uhusiano yanayohitaji kutambuliwa mapema. Kuzielewa kunaweza kusaidia kuchukua hatua stahiki kabla hali haijawa mbaya zaidi.
