Wadau waiangukia SMZ kuhusu viwanja

WADAU wa michezo Zanzibar, wamesema viwanja vinavyoendelea kujengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) vinapaswa kuwa mali ya umma na sio makundi machache yenye uwezo wa kifedha.

Wamesema endapo Serikali itafanya hivyo itakuwa imetekeleza lengo la kuinua sekta ya michezo na kutoa ajira kwa vijana tofauti na sasa ilivyo.

Akizungumza kuhusu uwekezaji huo wa viwanja unaofanywa na Serikali, mdau wa michezo kisiwani hapa aliyejitambulisha kwa jina la Mohammed Rashid, alisema hiyo ni hatua kubwa kwa jamii yenye kuamini fursa zitokanazo na michezo.

“Wachezaji wakubwa wanaowakilisha Taifa kwa sasa wametokea kwenye mazingira mabovu lakini juhudi zao na walimu wao zimewafikisha hapo walipo, hivyo waliopata fursa hii waitumie vizuri,” alisema.

Mohammed alisema, hiyo ni nafasi nzuri kwa wachezaji wa sasa wenye lengo la kufika mbali kimichezo kupata nafasi ya kucheza kwenye viwanja vyenye ubora na viwango vya kiamataifa.

Aliongezea hiyo ni hatua nzuri ambayo itasaidia kulinda dhamira ya kuendeleza michezo Zanzibar na kuhakikisha vipaji vya vijana vinaendelea kukua kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Said Mohammed alisema viwanja hivyo vinapaswa kuwa na usimamizi mzuri bila kuwa na upendeleo kwa makundi yenye uwezo wa fedha na ambayo hayana, hilo linaweza kudhoofisha lengo la kukuza michezo kwa wote.

Aidha, alipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa madaraja ya matumizi ya viwanja kwa kuweka gharama kulingana na aina ya mtumiaji.

Akitolea mfano wa madaraja hayo ikiwemo timu za vijana, shule, vikundi vya kijamii na mashindano ya kitafa na kimataifa ili kuhakikisha kila kundi linapata nafasi ya kutumia miundombinu hiyo kwa wakati sahihi.

Hatua hiyo imekuja baada ya wadau hao kulalamika kwamba, viwanja wanavyokwenda kuvitumia vina gharama kubwa wakitolea mfano Uwanja wa Mao Zedong matumizi yake kwa mchana ni wanapaswa kulipia kuanzia Sh100,000 hadi Sh150,000 wakati usiku inaanzia Sh150,000 hadi Sh200,000, kiwango ambacho hawawezi kukimudu, hivyo wameomba iwe nafuu.